Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kwamba mambo yote anayoyatamka hadharani juu ya utekelezaji wa miradi mikubwa zaidi ya maendeleo hapa nchini sio porojo za kisiasa bali ni dhamira yake ya kweli ya utekelezaji.
Ameyasema hayo Disemba, 20 2024 alipofungua maegesho ya gari ya kwanza ya ghorofa Malindi Zanzibar, Shehiya ya Mchangani, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi amesema kufanya hivyo ni kuonesha uongozi unaoacha alama na uzalendo pamoja na kuwahakikishia wananchi kwa kauli mbio inayosema “yajayo ni makubwa zaidi.”
Akiitaja miradi mengine mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kutekelezwa miaka ijayo chini ya uongozi wake, Rais Dk. Mwinyi amesema ni pamoja na mradi wa taxi za baharini ambapo ujenzi wa bandari za taxi hizo umeanza Maruhubi zitakazopakia na kushua abiria watakao tumia usafiri wa maji kuelekea maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kutumia taxi hizo badala ya usafiri wa nchi kavu wa daladala na usafiri mwengine, Mradi wa treni zitakazotumia barabra za lami kutoka Malindi mjini hadi Bububu, ujenzi wa barabra nne za juu zenye mapishano pamoja na ujenzi wa jeti kwa usafiri maji kwa ajili ya kuwasafirishia watalii wanaotembelea visiwa vidogovidogo.
Pia amewatoa hofu wananchi wa Mji Mkongwe kwamba Serikali inatekeleza miradi yake huku ikiwa na dhamira njema ya kuuendeleza urithi wa Kimataifa ikiwa na lengo la kuulinda mji huo na sio kuuharibu.
Amesema, uzinduzi wa maegesho ya magari Malindi, una nia ya kupunguza msongamano wa magari makubwa na madogo yanayoingia na kutoka Mji Mkongwe.
Pia, Dk. Mwinyi amebainisha kuwa mbali na maegesho hayo, ameeleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo inakusudia kujenga kituo cha kisasa cha mabasi ya abiria, pembezoni mwa maegesho ya gari Malindi, sabamba na ujenzi wa kituo kikubwa cha gari za abiria pamoja na kiwanja cha michezo kwa vijana.
Amefahamisha kupitia mradi wa “Big Z” Serikali pia inakusudia kujenga mradi wa barabara ya kisasa kutoka Malindi hadi hospitali ya Mnazi Mmmoja ikiwa ni hatua ya kuupandisha hadhi Mji Mkongwe pamoja na kuwa na mradi wa kuweka waya zote za umeme, maji na mawasiliano chini ya ardhi ili kuimarisha usafi wa mji huo kwa kuikarabati umpya kwa kuiboreshea haiba njema, bustani ya “Jamhuri garden” ili iwe na mwonekano wa kisasa.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kutekeleza wajibu wao wa kutoa mafao kwa wananchi kwa wakati na kwa kiwango kizuri, kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kufanikiwa kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi kwa kujenga miradi mikubwa, akitolea mfano mataifa mengine duniani kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ndio inayojenga nchi, hivyo aliitaka ZSSF kuendeleza utaratibu huo.
Dk. Mwinyi pia amewasisitiza wanachi kuendelea kuidumisha amani ya nchi, umoja na mshikamano ili nchi iendelee kupiga hatua kubwa za maendeleo.