Home KITAIFA RAIS DK. MWINYI: KUSHUKA KWA THAMANI YA DOLA KUTAPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA

RAIS DK. MWINYI: KUSHUKA KWA THAMANI YA DOLA KUTAPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA

Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kushuka kwa thamani ya dola nchini ni faraja kubwa kwa Uchumi kwani kutapunguza ugumu wa gharama za maisha kwa wananchi.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Disemba, 19 2024 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba pamoja na ujumbe wake waliomtembelea.

Rais Dk. Mwinyi amesema, ni matarajio yake kushuka kwa dola kutasaidia pia kupungua gharama za baadhi ya mahitaji kwenye maisha ikiwemo bidhaa muhimu chakula na mafuta.

Amebainisha kuwa bidhaa zote zilizoathirika kutokana na kupanda kwa dola duniani ni matarajio yake zitarejea kwenye uhalisia wake.

Akizungumzia suala la uingizwaji wa bidhaa nyingi na athari za kupanda kwa dola, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba iliathiri sana Uchumi wa nchi licha ya kuwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zilifidia hasara hasa wakati wa mavuno akitolea mfano chakula ikiwemo mchele kwa kiasi ilipunguza kasi ya uagiziaji kutoka nje.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa weledi wa kuendelea kuwahamasisha wananchi juu ya kubadilisha noti za zamani zinazoondoshwa kwenye mzunguko kwa matumizi yao ya kila siku.

Amahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na Benki hiyo ili kushajihisha jamii na kuwajengea uelewa wananchi wa kubadili noti za zamani kusaidia kuondoka kwenye mzunguko kwa wakati.

Naye, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ( BoT), Emmanuel Tutuba amemueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Benki hiyo inaendeleza zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za shilingi 20, 200, 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003.

Amesema Benki hiyo pia imetoa muda maalumu kwa Watanzania kuanzia Januari 2025 hadi Aprili 2025 kuutumia kubadilisha noti za zamani kupitia Ofisi zote za Benki Kuu ya Tanzania na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kinachobadilishwa.

Aidha, Gavana Tutuba ameeleza matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania ifikapo Aprili 06 mwaka 2025 na kusisitiza kuwa baada ya tarehe hiyo noti hizo hazitatumika kwa matumizi yoyote popote duniani.

Pia, ametoa rai kwa wananchi wenye noti za zamani kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi kilichowekwa.

Akizungumzia kuhusu kushuka kwa thamani ya dola nchini, Gavana Tutuba amesema ni hatua moja ya Benki hiyo kuipandisha thamani na kuirejesha kwenye mzungungo wa soko, fedha ya ndani ambayo kwa kipindi kirefu ilishuka, hivyo ametoa indhari kwa wafanyabishara wote nchini pamoja na kuwajuulisha Watanzania kwamba ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kuuza ama kununua bidhaa kwa kutumia dola ama fedha yoyote ya kigeni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here