Dar es Salaam
MWINJILISTI wa Kimataifa, Alphonce Temba amewataka viongozi wa Kisiasa kusimamisha wagombea wanaothamini amani na umoja uliopo nchini.
Pia amevitaka vyama vya upinzani kuacha tabia ya kubeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeweza kutunza amani iliyopo nchini kwa siku nyingi.
Akizungumza na waandishi wa habari Disemba,15 2024 jijini Dar es Salaam Temba amesema siku zote amani ya nchi inavunjwa na wanasiasa wasiojua siasa na wale wenye matamshi ambayo yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Temba alisema mwanasiasa yeyote anatakiwa kuwa na lugha fasaha ambayo haitaleta kichocheo chochote ndani ya jamii.
Aidha katika mkutano huo Mwinjilisti huyo amemsifia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji wake wa kazi na kuleta maridhiano mazuri ndani ya vyama vya siasa.
“Si kazi ndogo aliyoifanya ya kuleta maridhiano kwa vyama vya siasa vilivyopo nchini ambavyo hadi leo hii tunaviona jinsi vinavyoshirikiana katika mikutano mbalimbali ya kimataifa na kuweza kufanya mikutano yao ya hadhara ambapo hapo awali kulikuwa hakuna kitu kama hicho,”amesema.
Pia Mwinjilisti Temba amewataka viongozi wa kisiasa kuyaona mazuri yanayofanywa na Serikali ikiwemo kukuza viwanda nchini na vijana kupata ajira.
Katika mkutano huo Mwinjilisti amemuonya mgombea wa nafasi ya Uenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kuacha kutoa maneno ya kejeli kwa Mwenyekiti aliyopo madarakani kwa sasa Freeman Mbowe kwa kusema kuwa hana uwezo tena wa kukiongoza chama hicho.
“Namshangaa Tundu Lisu kwa maneno anayotoa ya kubeza uongozi wa Mbowe,hakumbuki kwamba Mbowe ndiyo aliyemshikia drip ya damu hadi Nairobi Kenya wakati aliposhambuliwa kwa kupigwa risasi”?amehoji Temba mbele ya waandishi wa habari.