Dar es Salaam
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi katika Ofisi ndogo za Wakala ya Barabara (TANROADS), leo Disemba, 11 2024 Dar es Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, pamoja na Wakuu wa Taasisi kutoka Wakala ya Barabara (TANROADS), Wakala wa Majengo (TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT).
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Ulega amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumteua kuhudumu katika Wizara ya Ujenzi.
Aidha, ameahidi kuwapa ushirikiano Wakuu wa Taasisi hizo na kuendeleza yale yote ambayo yapo katika utekelezaji yakiwemo majukumu makuu ya Wizara ya Ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, ujenzi na usimamizi wa vivuko, ujenzi wa majengo na nyumba za watumishi na Viongozi wa Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour amemkaribisha Waziri Ulega na kumuahidi ushirikiano kutoka kwa Menejimenti na watumishi wa Wizara pamoja na Taasisi zake.