Home KITAIFA TUENDELEE KUTUMIA TEKNOLOJIA KATIKA SHUGHULI ZA UHIFADHI – DK. ABBASI

TUENDELEE KUTUMIA TEKNOLOJIA KATIKA SHUGHULI ZA UHIFADHI – DK. ABBASI

Na Joyce Ndunguru, Morogoro

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi ameelekeza kuendelea kwa matumizi ya teknolojia mbalimbali katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori.

Dk. Abbasi ameyasema hayo Disemba 10, 2024, katika kikao na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kilichofanyika katika Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro.

“Tuendelee kutumia teknolojia za kisasa katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori “, amesema Dk. Abbasi.

Aidha, ameipongeza TAWA kwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma mnamo mwezi Septemba ya kununua ndege nyuki kwa ajili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

“Nimefurahi kuona mmeanza kutekeleza maelekezo ya Rais ya kununua ndege nyuki na hapa TAWA nimeona kazi imeanza” ameongeza Dk. Abbasi

Vilevile, ametoa pongezi kwa TAWA kwa ujenzi wa vizimba sambamba na ujenzi wa mabwawa katika Hifadhi ya Rungwa na Makuyuni ambao utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wanyamapori. 

Kwa upande wake, akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange amemshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwa asilimia mia moja

” Sisi kama TAWA ni jadi yetu kutekeleza maelekezo bila kupindisha,” amesema Kamishna Kabange.

Kuhusu matumizi ya teknolojia, Kamishna Kabange ameongeza kuwa TAWA imenunua ndege nyuki 11 kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na itaongeza nyingine zaidi, sambamba na kutafuta teknolojia zingine zitakazosaidia katika shughuli za uhifadhi.

Awali, Dk.Abbasi alipata wasaa wa kuangalia onesho la matumizi ya ndege nyuki katika kumrudisha tembo hifadhini sambamba na kukabidhiwa kombe la SHIMMUTA kwa upande wa mashindano ya Kamba  na Riadha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here