Na Shomari Binda, Musoma
ZAHANATI mpya imefunguliwa Disemba, 5 2024 kwenye Kijiji cha Nyabaengere Kata ya Musanja Jimbo la Musoma vijijini ili kuendelea kuwafikia karibu wananchi na kutoa huduma.
Ujenzi wa zahanati hiyo ulianzishwa kupitia harambee iliyoanzishwa na mbunge wa jimbo hilo Profesa Sospeter Muhongo huku wananchi wakichangia nguvu kazi na fedha.
Kata ya Musanja yenye vijiji vitatu vya Mabuimerafuru, Musanja na Nyabaengere haikuwa na zahanati hata moja huku wananchi wakilazimika kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za afya kwenye Kata jirani ya Murangi
Vijiji viwili vya Nyabaengere na Mabuimerafuru vinajenga zahanati za vijiji vyao na leo Kijiji cha Nyabaengere kimezindua utoaji na huduma za afya kwenye zahanati yake mpya.
Wakizungumza kijijini hapo wananchi wameshukuru juhudi za mbunge wao kwa kuanza na harambee hadi kufikia malengo.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho, Malima Mugeta amesema bila jitihada na uhamasishaji uliokuwa ukifanywa na mbunge Muhongo wasinge fanikiwa.
Malima amesema licha ya hamasa ya mbunge aliwachangia mifuko 100 ya saruji ambayo ilikuwa sehemu ya ujenzi huo.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Muhongo imeeleza kuwa diwani na wanakijiji thamani ya michango yao ni takribani shilingi milioni tano.
Wazaliwa wa Kijiji cha Nyabaengere wamechangia jumla ya shilingi laki 400,000 halmashauri ya Musoma DC ilichangia shilingi milioni 50 na serikali kuu ilichangia shilungi milioni 50.
Wananchi ya Jimbo la Musoma Vijijini na viongozi wao wanaendelea kuishukuru serikali inayoongozwa vizuri na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuchangia fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.