Home KITAIFA WAZIRI MKUU AAGIZA MAPENDEKEZO YALIYOMO KWENYE TAFITI YA MHITIMU WA PhD ALIYEFARIKI...

WAZIRI MKUU AAGIZA MAPENDEKEZO YALIYOMO KWENYE TAFITI YA MHITIMU WA PhD ALIYEFARIKI KUFANYIWA KAZI.

Ni Tafiti kuhusu milipuko ya moto kwenye masoko ya Umma.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Idara ya Menejimenti ya Maafa na Jeshi la Zimamoto kutumia mapendekezo yaliyomo kwenye tafiti ya marehemu Billy Mwakatage ambaye ni mhitimu wa shahada ya Uzamivu (PhD) aliyefanya tafiti kuhusu majanga ya moto kwenye masoko ya umma.

Ametoa wito huo leo (lAlhamisi, Desemba 05, 2024 alipomwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango kwenye mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Kawawa, Manispaa ya Kigoma. Shahada hiyo ilipokelewa na Mjane wa Marehemu, Ningile Kapange.

Amesema kuwa tafiti hiyo ina mahusiano makubwa na shughuli inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa katika kudhibiti maafa na majanga mbalimbali.

“Kwa kuwa ameshahitimu na leo anapata shahada na amefanya utafiti wa kina kwenye eneo hili la maafa na hasa majanga ya moto ambayo wakati wote Serikali tumekuwa tukipambana nayo, msomi wetu Marehemu Billy Mwakatage pamoja na utafiti ametoa mapendekezo mbalimbali, chukue utafiti huu na muufanyie kazi katika kukabiliana na majanga hapa nchini,”amesema.

Tafiti ya Marehemu Billy Mwakatage alifanya tafiti kuhusu “mambo yanayoathiri na nia ya kuzuia milipuko ya moto katika soko la umma nchini Tanzania”.

Katika hatua nyingine Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuandaa mpango wa mafunzo kwa wahadhiri nchini ili wapate fursa za kufanya tafiti kwa kushirikiana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Pia, ameiagiza Wizara hiyo kuandaa mpango mahsusi wa kukuza kazi za ubunifu na iweke mkakati wa kuwezesha kuuza bunifu hizo.

“Kama mnavyofahamu ubunifu ni biashara. Pia, ubunifu unazalisha ajira na kuongeza kasi yamaendeleo ya Taifa,”amesema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here