Home KITAIFA BASHUNGWA AITAKA JUMUIYA YA WAHASIBU WAKUU AFRIKA KUWEKA MIFUMO YA USIMAMIZI WA...

BASHUNGWA AITAKA JUMUIYA YA WAHASIBU WAKUU AFRIKA KUWEKA MIFUMO YA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

Arusha

JUMUIYA ya Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika wametakiwa kuandaa mapendekezo yanayohusu umuhimu wa mifumo madhubuti ya usimamizi wa fedha za umma inayoweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza duniani ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya kiteknolojia na mabadiliko ya kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa jijini Arusha leo Disemba 02, 2024 wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (AAAG) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha ambao umebeba kauli mbiu isemayo “Kujenga Imani ya Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu”.

Bashungwa amesisitiza kuwa uwepo wa matumizi ya mifumo thabiti itapunguza gharama za usimamizi, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Jumuiya hiyo kupendekeza mbinu mpya za kuboresha usimamizi wa fedha za umma kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

“Kuboresha ufanisi na uwazi wa matumizi ya fedha za umma utasaidia katika kupunguza rushwa, kuongeza uaminifu wa umma katika mifumo ya kifedha pamoja na itaongeza uwezo wa kutunza na kufuatilia matumizi ya fedha na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa wadau”, ameeleza Bashungwa.

Vilevile, Bashungwa ameitaka Jumuiya hiyo kuona namna ya kukuza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Asasi za kiraia, katika usimamizi wa fedha za umma hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo endelevu ili isaidie ufanisi na uthabiti katika utekelezaji wa miradi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ameeleza usimamizi madhubuti wa fedha unasaidia wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri.

Nchemba amethibitisha hayo kwa kutolea mifano ya miradi iliyokamilika na inayotekelezwa nchini ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme, miradi ya umwagiliaji, miundombinu ya barabara, ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo – Busisi) pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Naye, Mhasibu Mkuu wa Serikali wa Ufalme wa Lesotho na Mwenyekiti wa Jumuiya ya AAAG, Malehlonolo Mahase ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo kuna malengo na manufaa muhimu katika usimamizi bora wa fedha za umma na kuimarisha utendaji katika nchi za Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here