Arusha
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro.
Pia amesema Tume nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongo.
Rais Dk.Samia ameyasema hayo leo Desemba,01 2024 Ikulu ndogo jijini Arusha wakati akizungumza na viongozi wa Kimila wa Jamii ya Kimasai (Malaigwanani) wanaoishi katika eneo la Ngorongo.
Amesema mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya serikali yanayohusu eneo la Ngorongo.
“Nawahakikishia kuwa serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongo (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya serikali na jamii hii,” amesema Dk.Samia.
Amesisisitiza kuwa kuna ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji wa miradi inayopita kwenye maeneo yao.
Rais Dk.Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye serikali inayowahudumia watanzania wote.
Hata hivyo ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongo.