Home KITAIFA MAKAMU WA RAIS MSIBANI KWA DK. NDUGULILE

MAKAMU WA RAIS MSIBANI KWA DK. NDUGULILE

Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango amesema marehemu Dk. Faustine Ndugulile alikua kiongozi mwenye nidhamu, rafiki wa kila mtu na kiongozi aliyeweza kutetea vema maslahi ya Taifa.

Dk. Mpango amesema hayo leo Novemba, 30 2024 alipofika nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dk. Faustine Ndugulile Kigamboni Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuifariji familia pamoja na waombolezaji wote.

Amewaombea faraja na moyo wa uvumilivu wote walioguswa na msiba huo. Amewashukuru wote walioshiriki katika kuifariji familia wakati huu wa kipindi kigumu kwao na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana katika nyakati mbalimbali zinazojitokeza katika jamii ikiwemo za majozi na furaha.

Aidha amesema inapaswa kuendelea kumshukuru Mungu kwa maisha ya Dk. Ndugulile hapa duniani. Ameongeza kwamba ni vema kwa Watanzania kuendelea kuishi vizuri na ndugu na majirani.

Akiwa nyumbani hapo, Makamu wa Rais amesali pamoja na familia, ndugu, jamaa na marafiki kumuombea marehemu Dk. Faustine Ndugulile.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here