Home KITAIFA USALAMA WA BAHARINI UNA MUHIMU KWA UCHUMI WA DUNI

USALAMA WA BAHARINI UNA MUHIMU KWA UCHUMI WA DUNI

Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Antonio Dominguez amesema usalama wa baharini una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa dunia kwani unabeba ustawi wa mazingira na jamii kote ulimwenguni.

Kauli hiyo imetolewa Novemba, 28 2024 jijini Dar es Salaam,amesema bila jitihada kufanyika katika kutokomeza suala hilo ni ngumu kupata bidhaa, huduma na hata misaada ya kibinadamu ambayo ni muhimu kwa maisha ya mabilioni ya watu duniani.

“Tukizingatia mashambulizi yanayoendelea dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu (red sea) yanahatarisha usalama wa wanamaji, utulivu wa biashara ya baharini, na usalama wa kanda. Ninakaribisha mbinu ya Kamati ya Uongozi katika kutafuta suluhisho la kikanda kwa changamoto hii ya dharura,” amesema Dominguez.

Amesema hatua ambazo zimefanywa katika kuratibu shughuli kwa uhsirikiano na washirika wa kimataifa ni mfano unaohitajika katika kukabiliana na vitendo hivi vinavyoongezeka.

“Pia, ni lazima tuhakikishe juhudi hizi za pamoja zinaendelezwa na kuimarishwa ili kulinda njia zetu za baharini na kuepuka kurudi kwa ukosefu wa amani kama ilivyokuwa wakati wa migogoro ya uharamia hapo awali,” amesema.

Amesema mbali na uharamia pia alitaka uhalifu mwingine kutopuuzwa ikiwemo ule wa magendo, uchafuzi wa bahari sambamba na biashara haramu ya binadamu na wanyamapori.

“Pia uwepo wa vitu vipya kama kama mashambulizi ya mtandaoni, matumizi ya ndege zisizo na rubani vitu hivi vinahitaji tahadhari yetu ya mara kwa mara na hatua za pamoja,” amesema.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa zikiathiriwa na uharamia unaofanywa katika maeneo mbalimbali ya bahari kutokana na kuongezeka kwa gharama za bidhaa.

“Mfano, mfereji wa Suez Canal unakadiriwa kupitisha asilimia 10 ya biashara ya kimataifa na takribani asilimia 22 ya kontena zote.

Aidha inaelezwa kuwa kuwapo kwa uharamia unaofanyika, watu wanapolazimika kubadilisha njia huongeza mahitaji ya meli za kontena kwa asilimia 12.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema changamoto ya uharamia iliyokuwapo katika eneo la bahari nyekundu mwaka jana yalikuwa na athari.

“Miongoni mwa athari ni watu kuuwawa jambo ambalo liliweka mashaka na watu kulazimika kupita njia ya mbali jambo ambalo liliongeza gharama za uendeshaji meli kwa kutumia mafuta mengi.

“Jambo hili lilifanya bei za vitu ikiwemo vyakula na mafuta kupanda. Sasa serikali zote hasa katika ukanda wa red sea, Guba ya Aaden, Djibouti kuamua kuwa tunaweka mkakati wa kupambana na maharamia wa meli ili bahari iwe salama kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafirishaji,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema kufanya hivyo kunasaidia biashara kuwa nzuri na wananchi wanapata bidhaa zao kwa bei nafuu zaidi.

“Uharamia ukitokea hatupambani Tanzania pekee bali tunasimama kama jumuiya kwa sababu wengine wana meli zinapita na sisi tunahitaji mahitaji yetu sasa kadri uharamia unavyokuwa mkubwa hata meli mbalimbali haziwezi kufika na zile zitakazofanikiwa zikija na bidhaa bei itakuwa kubwa zaidi ndiyo maana jambo hilo linafanyika,” amesema.

Amesema jumuiya yote ya nchi zilizopo maeneo hayo hushirikiana kwa pamoja kupambana na maharamia ikiwemo meli za kimarekani zile za vita ili kuweka urahisi katika mapambano hayo.

“Kilichopo ni kwamba kila teknolojia ikibadilika na wao wanakuja na mbinu mpya za uharamia hivyo inailazimu jumuiya hii kukaa kila wakati kuangalia kile kilichofanyika ni kwa kiasi gani kinahitaji maboresho,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here