Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi asema idadi ya washiriki wa Mkutano huo imevunja rekodi kwa wingi wake
• Maeneo matano kujadiliwa ili kuboresha huduma ya utoaji haki katika ukanda huo
Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa 21 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) utakaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 02 hadi 07 Desemba, 2024.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wa mkoani Arusha leo Novemba, 28 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kuhusu maandalizi ya Mkutano huo, Jaji wa Makahama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo,Dk. Gerald Ndika amesema kuwa, Mkutano huo utafanyikia katika Hoteli ya Gran Melia’ jijini humo.
“Ndugu Wanahabari napenda kuchukua nafasi hii kuwajulisha kuwa, katika Mkutano wa Mkuu uliopita Mahakama ya Tanzania ilipewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki kwa mwaka huu,” amesema Dk. Ndika.
Jaji Ndika amesema kwamba, mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa tarehe 03 Desemba, 2024 na Rais Dk. Samia na unatarajiwa kuhudhuriwa na jumla ya washiriki 392 kutoka Uganda, Kenya, Rwanda, Zanzibar na Sudani ya Kusini.
“Muitikio ni mkubwa sana kwa mwaka huu na ninaweza kusema kuwa idadi imevunja rekodi,” amesema Jaji Ndika.
Dk. Ndika ameongeza kuwa, katika Mkutano huo kutakuwa na maeneo/mada tano ambazo zitakazojadiliwa mojawapo ni eneo la uboreshaji wa Mifumo ya Utoaji Haki, kuangalia namna bora ya kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi, utoaji wa haki katika migogoro ya kazi, hatua ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama za ukanda huo na kadhalika.
“Mkutano huu wenye kaulimbiu isemayo ‘Uboreshaji wa Mifumo ya Utoaji Haki kwa ajili ya kuimarisha Utengamano na Ukuzaji Uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC)’ utaangazia maeneo matano ambapo Desemba 3 hadi 4 tutajadili programu za maboresho ya mifumo ya utoaji haki jinai kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa utoaji wa haki jinai, programu za utoaji haki katika mfumo wa madai ikiwemo mirathi, ajira, mikataba, ikiwemo uboreshaji wa utoaji haki katika madai,” ameeleza Dk. Ndika.
Ameongeza kuwa, eneo lingine ni la uboreshaji wa utoaji haki katika migogoro ya kazi kwani migogoro ya kazi inahusu pia Baraza la usuluhishi na ni eneo muhimu kwakuwa kuna migogoro mingi baina ya mwajiri na mwajiriwa na ikisikilizwa mapema inaongeza imani kwa wawekezaji na kuvutia wawekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika utoaji haki, Jaji Ndika amebainisha kuwa, kwa upande wa Tanzania, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA ambapo kwa sasa kuna mifumo mbalimbali inayorahisisha utoaji wa haki nchini.
“Sasa hivi tunafanya usajili wa mashauri kwa kutumia mtandao lakini pia tunasikiliza mashauri mengi kwa njia ya mtandao, vilevile tuna mfumo wa kurekodi mwenendo wa mashauri (TTS) ili kumpunguzia kazi Jaji au Hakimu kuandika kwa mkono ikiwemo kutoa tafsiri kwa lugha ya kingereza na kiswahili ili kuongeza ufanisi zaidi ikiwemo uchapishaji uamuzi kwa njia ya mtandao,” amesema Dk. Ndika
Chama cha Mahakimu na Majaji wa Afrika Mashariki (EAMJA) kilianzishwa mwaka 2000 na kuzinduliwa mwaka 2001 nchini Uganda, malengo ya Chama hicho ni pamoja na kuwapa jukwaa Majaji na Mahakimu kujadili changamoto, mafanikio na kupeana uzoefu ikiwemo kutetea na kulinda uhuru wa Mahakama za Afrika Mashariki (EAC).
Akitoa neno la utangulizi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), John Kahyoza amesema JMAT ilianzishwa mwaka 1984 na miongoni mwa madhumuni ya uanzishwaji wa Chama hicho ni kutumika kama jukwaa la kujadili utendaji kazi wa Majaji na Mahakimu, kusimamia uhuru wa Mahakama na mengine.