Home KITAIFA WATUHUMIWA SABA MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA, DCEA YAKAMATA...

WATUHUMIWA SABA MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA, DCEA YAKAMATA TANI 2.2 ZA DAWA

Dar es Salaam

MAMLAKA  ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imekamata jumla ya kilogramu 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari na kwamba watuhumiwa saba wanashikiliwa kuhusiana na dawa hizo. 

“Kati ya dawa zilizokamatwa, skanka ni kilogramu 1,500.6, methamphetamine kilogramu 687.76, heroin kilogramu 19.20, na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Mnamo Novemba 14, 2024, jijini Dar es Salaam, katika wilaya ya Kigamboni, mtaa wa Nyangwale, watuhumiwa Mohamed Suleiman Bakar (40) na Sullesh Said Mhailoh (36), wote wakazi wa Mabibo, Dar es Salaam, walikamatwa wakiwa na kilogramu 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya skanka.

Kamishna Jenerali Lyimo ameeleza kuwa Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga mtuhumiwa Mohamed, ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo. 

Amesema dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajili T 534 EJC, zikiwa tayari kwa kusambazwa. 

Ameongeza kuwa tarehe hiyo hiyo, katika mtaa wa Pweza Sinza E, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa Iddy Mohamed Iddy (46), mkazi wa Chanika Buyuni, alikamatwa akiwa na kilogramu 150.2 za skanka, zilizokuwa zimefichwa katika maboksi ya sabuni na baadhi ya dawa hizo zikiwa zimefichwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati ngumu na kupachikwa kwenye chassis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini LN87XJGP, ambalo limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi. 

Vilevile, amesema Novemba 17, 2024, katika jiji la Tanga, watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahadi Ally Kassim (36) walikamatwa mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilogramu 706.96 za dawa aina ya heroin na methamphetamine. 

Kwamba baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 714 EGX, huku nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga mtuhumiwa.  

Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa Novemba 19, 2024, katika mtaa wa Kipata na Nyamwezi Kariakoo jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Michael Dona Mziwanda (28) mkazi wa Tabata Segerea, na Tumpale Benard Mwasakila (32) mkazi wa Temeke Mikoroshini, walikamatwa wakiwa na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl wakiwa nazo katika duka la M-PESA. 

Amesema, katika operesheni hizo zilizofanyika, jumla ya magari matatu na Boti moja vilivyohusika katika uhalifu huo vinashikiliwa. 

“Dawa zilizokamatwa ni nyingi na zingeweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii na Taifa ikiwa zingeingia mitaani. Dawa hizi haziathiri tu wale waliokwisha anza matumizi ya dawa za kulevya, bali pia wafanyabiashara hawa hulenga watu wengine ambao hawajaanza matumizi ili kutanua masoko yao,” ameeleza Kamishna Jenerali Lyimo na kuongeza,

“Walengwa wapya wanaweza kuwa mtu yeyote katika jamii au familia za Kitanzania. Hivyo, ni dhahiri kuwa jamii nzima inakabiliwa na hatari ya dawa za kulevya,”.

Amebainisha kwamba Mamlaka imebaini kuwa wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya hutumia mbinu ya kupanga nyumba ambazo zinageuzwa kuwa maghala ya kuhifadhi dawa za kulevya, huku wao wakiishi katika maeneo mengine. 

Ametoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini wanapopangisha nyumba zao, kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa. 

Ameeleza kuwa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba, msimamizi wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza, kuvuta, kujidunga, kuuza au kununua dawa za kulevya. 

Aidha, mmiliki anapojua kuwa kosa linatendeka kwenye eneo lake, anajukumu la kutoa taarifa kwa Mamlaka kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai, na akitiwa hatiani, adhabu yake inaweza kuwa faini kuanzia shilingi milioni tano hadi milioni hamsini, au kifungo cha miaka mitano hadi miaka thelathini jela, au vyote kwa pamoja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here