Home KITAIFA CHALAMILA:TAARIFA YA AJALI YA JENGO LA KARIAKOO ITATOLEWA NA MSEMAJI MKUU...

CHALAMILA:TAARIFA YA AJALI YA JENGO LA KARIAKOO ITATOLEWA NA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa taatifa rasmi kuhusu ajali ya jengo lililoporomoka katika eneo la Kariakoo na kusababisha vifo vya watu 20 inatarajia kutolewa hivi karibuni na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila

Akizungumza leo Novemba, 25 2024 jijini Dar es Salaam Chalamila amesema Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba atatoa taarifa hiyo kwa kibali maalumu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Tunatambua kuwa wananchi wanahitaji taarifa kamili juu ya tukio hili la kusikitisha Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina na taarifa itatolewa rasmi ili kuweza wazi hatua zilizochukuliwa,” amesema.

Amesema taarifa hiyo itahusisha mchakato mzima wa ubomoaji jengo hilo na hali ya waathirika waliopona katika ajali hiyo Novemba 16, 2024.

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Chalamila ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi siku ya Novemba 27,2024 kupiga kura na kuchagua viongozi kwani uchaguzi huo utakuwa na amani na utulivu na jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha utulivu na amani vinapatikana wakati watu wa zoezi hilo.

Amesema hali ya usalama kwa mkoa ipo vizuri na yeyote atakae haribu hali hiyo hataachwa salama bali hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Niwatoe wasiwasi wananchi jitokezeni mkapige kura na mkimaliza nendeni kwenye majukumu yenu askari wapo kila sehemu tena wakutosha watalinda amani,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna uwepo wa 4R za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan zenye kuhimiza ustahimilivu unaongeza chachu kwa taifa hivyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi itapelekea nchi kuvuka kihunzi kwenye maswala ya demokrasia

“Uchaguzi si kipimo cha demokrasia bali uchaguzi huo unapaswa kuwa huru na haki lakini unaoakisi zile 4R ambazo Rais Dkt Samia ameziasisi,”amesema.

“Kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya viongozi walienguliwa kwenye mchakoto lakini kuna Vyama vingi sana vimeshiriki na vimesimamisha wagombea katika maeneo mbalimbali hivyo ni matumaini yetu wale wapenzi wa vyama vingi tarehe 27,watashiriki uchaguzi ili kuchagua viongozi wanaowataka,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here