Home AFYA WAUGUZI IDARA YA CHUMBA CHA UPASUAJI MOI, MNH, AGAKHAN NA TEMEKE WANOLEWA

WAUGUZI IDARA YA CHUMBA CHA UPASUAJI MOI, MNH, AGAKHAN NA TEMEKE WANOLEWA

Dar es Salaam

WAUGUZI wa Idara ya chumba cha upasuaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH_Mloganzila), Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Temeke na Hospitali ya Agakhan wajengewa uwezo namna ya kuwasaidia madaktari wakati wa kufanya upasuaji wa mivunjiko ya mifupa.

Mafunzo hayo yametolewa leo Jumamosi Novemba 23, 2024 katika taasisi ya MOI yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wauguzi namna ya kuwasaidia madaktari kufanya upasuaji wa mivunjiko ya mifupa.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Daktari Bingwa na Mbobezi wa Upasuaji wa Mifupa wa MOI, Dk. Adam Hussein amewakumbusha wauguzi hao kuzingatia kanuni na misingi ya kutoa huduma na kuwaandaa wagonjwa kabla ya kuwafanyia upasuaji wa mifupa hasa wagonjwa wa mivunjiko itokanayo na ajali.

“Wauguzi mna kazi kubwa ya kuwasaidia Madaktari hususani kabla, wakati na hata baada ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliovunjika mifupa, mfano wale wa ajali za barabarani au wale waliopata ajali ya kudondokewa na majengo,”amesema Dk. Adam na kuongezea

“Mnatakiwa mfanye kazi kwa kuzingatia kanuni, misingi na miongozo ili muweze kutoa huduma hizi za upasuaji wa mifupa kwa weledi na usahihi zaidi,”amesema.

Awali akifungua mafunzo hayo, Muuguzi Mwandamizi chumba cha upasuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH_Mloganzila), Adonis Mshanjara amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa na kufadhiliwa na shirika lisilo la Kiserikali liitwalo AO Alliance kutoka nchini Uswizi ambalo hufadhili mafunzo ya mivunjiko ya mifupa kwa Hospitali zinazotoa huduma za upasuaji wa mivunjiko ya mifupa.

“Ni matarajio yetu kuwa baada ya mafunzo haya, huduma za upasuaji wa mifupa kwa wagonjwa katika hospitali zilizoshiriki mafunzo haya, wagonjwa watakwenda kupata huduma bora za matibabu ya upasuaji wa mifupa” amesema Mshanjara

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here