Dar es Salaam
WAGONJWA na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamehimizwa kudai risiti baada ya kufanya malipo.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 22, 2024 na Meneja Utawala wa MOI, Amir Mkapanda, wakati wa kusikiliza kero, changamoto, maoni na pongezi kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.
Mkapanda amesema kuwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanatakiwa kudai risiti mara tu baada ya kufanya malipo kwa ajili ya huduma za matibabu kwani hiyo ni haki yao.
“Jamani risiti ni haki yenu, mkishafanya malipo kwa ajili ya kupata huduma za matibabu daini risiti, hiyo ni haki yenu, mkikwama sisi viongozi tupo tutawasaidia na mtapata haki yenu,”amesema Mkapanda
Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa Juma Ismail kutoka Mkurunga mkoani Pwani, amewapongeza Madaktari kwa namna walivyomtibu mgonjwa wake, kwani hali yake inazidi kuimarika kila siku.
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake, imetenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kusikiliza kero, changamoto, maoni na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.