Home KITAIFA AJIRA ZIPO, JIENDELEZENI KITAALUMA: KASEKENYA

AJIRA ZIPO, JIENDELEZENI KITAALUMA: KASEKENYA

Morogoro

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) kujiendeleza kitaaluma ili wawe na sifa stahiki zitakazowawezesha kushindana kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Mahafali ya Pili ya ICoT mjini Morogoro Novemba 21, 2024 Kasekenya amesema Serikali imejipanga kuiendeleza na kuiboresha Taasisi hiyo kimiundombinu na rasilimali watu ili iweze kutoa wataalamu wa msingi watakaotumika katika ujenzi wa miundombinu bora nchini katika miradi mbalimbali.

“Msiridhike na utaalamu mlionao, jiendelezeni siku kwa siku ili muwe na weledi unaoendana na Soko la mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia,”amesema Mhandisi Kasekenya.

Amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imejipanga kuifanya ICoT kuwa kitovu cha uzalishaji wataalamu bora wa Ujenzi, mafundi makenika, umeme, bomba, uchomeleaji na wataalamu wa barabara ili kuleta tija katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Amezungumzia umuhimu wa Taasisi hiyo kuwa na Programu za mafunzo ya muda mfupi yanayoendana na mahitaji ya soko ili kuongeza mapato ya Taasisi na kuongeza wataalamu wa fani mbalimbali katika soko la ajira.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya ICoT, Mhandisi Henry Paul Nyanga ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa juhudi zake katika kujenga jengo la taaluma la ghorofa nne ambalo likikamilika litaiongezea Taasisi hiyo uwezo wa kudahili wanafunzi wengi na kuiwezesha kukua kimiundombinu.

Ameongeza kuwa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICOT) ni muunganiko wa kilichokuwa Chuo cha Ujenzi Morogoro na Taasisi ya Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi ya Mbeya lengo lake ni kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali za Ujenzi watakaotumika katika miradi ya Ujenzi nchini.

Takriban wahitimu 231 wa fani za Uhandisi Ujenzi, Mitambo, Umeme, Uchoraji wa ramani za nyumba, Ufundi bomba na Uchomeleaji wamehitimu ngazi ya Stashada na Astahada na hivyo kuwafanya kuwa mafundi Sanifu na Mafundi Mchundo katika Fani hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here