Home KITAIFA ”RAIS SAMIA AUMIZWA MAUAJI YA KIBIKI”

”RAIS SAMIA AUMIZWA MAUAJI YA KIBIKI”

Simanzi yatanda mazishi yake

Nchimbi: matukio ya kutia hofu na shaka, hayakubaliki

Iringa

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ‘ameumizwa na kusikitishwa sana’ na tukio la kuuwawa kwa Ndugu Christina Alex Kibiki, aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi alipokuwa akitoa salaam za rambirambi na pole za Dk. Samia wakati wa mazishi ya Kibiki, yaliyofanyika katika eneo la Banavanu, Tosamaganga, Iringa vijijini, leo Ijumaa, Novemba,15 2024.

Kibiki alipoteza uhai usiku wa Novemba, 2024, baada ya kuvamiwa na kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake usiku huo, na watu wambao hawajajulikana hadi sasa, huku vyombo vya dola, kupitia jeshi la polisi, vikitangaza kuanza kuwasaka kwa ajili ya hatua za kisheria.

“Nianze kwa kutoa salaam za pole na rambirambi za Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Alipokea taarifa za tukio hili kwa masikitiko makubwa sana.

“Mwenyekiti wa CCM ameumizwa na kusikitishwa sana na tukio la mauaji haya ya mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi. Amenituma salaam za pole na rambirambi kwa familia, ndugu, wanaCCM na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa,” amesema Balozi Nchimbi.

Aidha, Balozi Nchimbi ameongeza kuwa tukio hilo na mengine ya aina hiyo, hayakubaliki na yanapaswa kupigwa vita na watu wote ili yakomeshwe mara moja nchini.

“Kitendo hiki alichofanyiwa marehemu Kibiki, ambapo mbali ya kumpiga risasi, wakamvunja mikono yote miwili na kumpiga na kitu kizito, na matendo mengine ya namna hii hayakubaliki na yanapaswa kukomeshwa mara moja. Yanaleta hudhuni, hofu, mashaka na kufanya maisha kutotabirika katika jamii ya wataarabu Tanzania,” amesema Balozi Nchimbi.

Akitoa salaam za Serikali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amesema kuwa serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria.

Amesisitiza kwamba hatua hii ni muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria na kudumisha amani na utulivu katika jamii.

Aidha, Serukamba amebainisha kuwa tangu tukio hilo litokee, serikali imepokea ushirikiano mkubwa kutoka kwa mikoa jirani pamoja na makao makuu ya polisi. Alisisitiza ushirikiano huu umeimarisha juhudi za uchunguzi, na mara tu uchunguzi utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa kwa umma kwa uwazi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin, ameonyesha imani kubwa kwa juhudi hizo za serikali, akisema, “Tunajua serikali ina mkono mrefu, na waliohusika katika tukio hili watahakikisha wananaswa.”

Aidha, ameongeza kuwa CCM kitaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wahusika wanawajibika kwa matendo yao hayo.

Mwenyekiti huyo pia aliwahimiza wananchi kuwa tayari kuonesha ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kwamba jukumu la kulinda usalama ni la kila mmoja katika jamii.

Shughuli hiyo ya mazishi ilitanguliwa na ibada na kuaga mwili wa marehemu Kibiki, katika Kanisa la Romani Katoliki, Tosamaganga, mkoani Iringa, ambapo misa iliongozwa na Padri Ernest Magelanga kwa niaba ya Paroko wa Parokia ya Tosamaganga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here