Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA)limesema jumla ya watahimiwa 557,731 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne ambao kati yao watahiniwa wa shule ni 529,321 na wakujitegemea ni 28,410.
Akizungumza leo Novemba, 10 2024 jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk.Said Mohamed amesema mtihani huo unatarajiwa kufanyika Novemba 11 hadi Novemba 29 mwaka huu katika jumla ya shule za sekondari 5,585 na vituo vya kujitegemea 961.
Amesema kati ya watahimiwa wa shule 529,321 waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.
Dk .Mohamed amesema jumla ya watahiniwa wa shule walio na mahitaji maalumu ni 1,088 ambao kati yao 601 ni wenye uoni hafifu, 56 ni wasioona, 209 wenye ulemavu wa kusikia ,39 ni wenye ulemavu wa akili na 183 wenye ulemavu wa viungo vya mwili.
“Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,410 waliosajiliwa, wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana ni 17,243 sawa na asilimia 60.69.
“Watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalumu wako 18, kati yao wenye uoni hafifu ni mmoja na wasioona ni 16 huku wenye ulemavu wa viungo ni mmoja ,”amesema.
Amesema mtihani wa kidato cha nne ni muhimu Kwa kuwa hupima umahiri wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne.
Aidha ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa kwani vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza mtihani la Tanzania.
Vilevile amewataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.
“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake,”amesema
Pia amesema wasimamizi hao wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanafanya upimaji wao ipasavyo ili wapate haki yao msingi ambazo ni pamoja na kupata mitihani yenye maandishi ya nukta nudu Kwa wanafunzi wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.
Kwa upande wa wanafunzi amesema Baraza la mitihani halitarajii kuona mwanafunzi yoyote kujiusisha na vitendo vya udanganyifu na kutoa taadhari kuwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.
“Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka miwili ya elimu ya sekondari na miaka minne ya elimu ya msingi,”amesema.
Aidha amewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mtihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huo.
Amesema baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo linajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa upimaji wa kitaifa.