Home MAKALA FFC KWAYA KUFANYA TAMASHA JNICC KUIKARIBISHA SIKUKUU YA KRISMAS KWA UIMBAJI WA...

FFC KWAYA KUFANYA TAMASHA JNICC KUIKARIBISHA SIKUKUU YA KRISMAS KWA UIMBAJI WA KIPEKEE

Dar es Salaam

DESEMBA 25 kila mwaka, Wakristo ulimwenguni kote usheherekea maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2000 iliyopita.

Sherehe hizo maarufu kwa jina la Krismasi huwaleta pamoja ndugu, jamaa na marafiki kukaa pamoja kwa kula na kunywa huku wakipeana zawadi mbalimbali.

Katika kuadhimisha sikukuu hiyo kwa mwaka huu, Kwaya Flying Family inayojumuisha waimbaji kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo wenye vipaji vya uimbaji wameamua kuendelea kuwa sehemu ya zawadi ya msimu wa sikukuu kwa kuwakutanisha wana wa Mungu na familia zao kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji wa nyimbo zenye ufundi wa hali ya juu.

Kwaya inajivunia kujenga umoja na upendo kwa wakristu kwa kutumia muziki na kuweza kuimba pamoja bila kujali tofauti zao za kimadhehebu kwa kipindi cha miaka sita sasa na kufanikiwa kuandaa matamasha makubwa saba yaliyowakusanya waumini na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali chini ya mchungaji mmoja Yesu Kristo.

Kwaya hiyo itafanya tamasha kubwa na wanakwaya wake kuimba ‘Classical music’ ambao ni maarufu duniani kote na umejizolea umaarufu tangu miaka ya zamani.

Innocent Fundisha ni Kiongozi wa kwaya hiyo anasema wapenzi wa muziki mtakatifu wakifika katika tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Desemba 15, mwaka huu katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jiini Dar es salaam watapata kusikia kazi za watunzi nguli kama George Handel, Wolfgang Mozart, Johan Bach, Joseph Haydn, Felix Mendelson, Anthonio Vivald na wengine wengi.

Hata hivyo anasema pia wanatumia kazi za watunzi wazawa kama David Wasonga, John Mgandu, Egidius Mushumbusi na Mathias Msafiri bila kusahau tenzi za rohoni.

Anasema tiketi za tamasha hilo zinapatikana Kanisa Katoliki la St Peter Osterbay, Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT) Msasani, Ofisi za Paones Posta Samora tower, KKKT Goba, Kanisa Katoliki Mwenge na Kanisa la Anglican Ilala. Kiingilio kitakuwa Sh. 50,000 kwa wakubwa, 30,000 kwa Watoto na 100,000 kwa VIP.

Pamoja na muziki mzuri siku hiyo kutakuwa na chakula na vinywaji vya kutosha kwa washiriki wote kama sehemu ya shangwe za msimu wa sikukuu.

Fundisha anasema si kazi rahisi kwa wanakwaya kujifunza nyimbo hizo lakini kwa msaada wa Mungu wanafanikiwa kushika na kujifunza kwa usahihi.

“Kwaya hii ilianzishwa Aprili, 2018 jijini Dar es Salaam ikiwa na wanakwaya wasiozidi 15 ila kwa sasa ina wanachama hai 40, tumeamua kumsifu Mungu na kutangaza sifa zake hapa duniani kwa njia ya uimbaji na kutumia muziki kudumisha umoja wa madhehebu ya kikristu,” anasema Fundisha.

Anasema anatambua kuwa sikukuu ya Krisimasi huwaleta pamoja na ndugu, jamaa na marafiki hivyo anaamini kupitia tamasha hilo watu wataburudika, watafurahi na kudumisha utamaduni wa kusheherekea Krismasi kwa njia ya muziki wa classical.

“Tunatarajia kuwa na Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo Kuu la Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwai’chi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, Askofu Jackson Sosthenes wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Dar es salaam.

“Pia tutakuwa na maaskofu wasaidizi Stephano Musomba na Henry Mchamungu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, mapadre na wachungaji. pamoja nao tutakuwa na ushiriki wa viongozi wa serikali pamoja na viongozi wastaafu, wanadisplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wakuu wa mashirika na taasisi za kiserikali na binafsi pamoja na washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania,” anasema

Lengo la kwaya hiyo

Fundisha anasema lengo la kuanzishwa kwa kwaya hiyo ni kuleta umoja na mahusiano mazuri katika madhehebu ya kikristo kwa njia ya kushirikishana vipaji vya kimuziki.

“Tunashirikishana vipaji hivyo vilivyopo kwa kuandaa kwaya ya pamoja, matamasha mbalimbali, huduma kwa wahitaji pamoja na kushiriki matukio ya kijamii yanayolenga kudumisha umoja wa wakristu na taifa kwa ujumla,” anasema Fundisha.

Anasema kwaya hiyo imeunda bodi ya wadhamini yenye wajumbe tisa wenye jukumu la kusimamia utendaji wa kwaya, kupanga mikakati ya Kwenda mbele zaidi na kuhakikisha malengo ya kwaya yanakuwa endelevu.

Anasema Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Eng. Anastas Mbawala, Dk. Emmanuel Manase, Chancellor Fr. Dr. Vincent Mpwaji, Mama Rose Rupia, Rev. Boniface Kombo, Vicar General Fr. Richard Kamenya, Fr. Michael Ndawile, Prof. Alex Makulilo na Mama Miriam Solomon

Utendaji kazi wa kikundi

Anasema kwaya inafanya mazoezi mara moja kwa wiki siku ya jumapili kuanzia saa tisa alasiri hadi saa kumi na mbili jioni, ili kutoa nafasi kwa wanakwaya wake ambao kila mmoja wao anahudumu kwenye kwaya yake kwenye usharika au parokia anakotokea na wanafanya mazoezi Katikati ya wiki na kuhudumu jumapili asubuhi.

“Hivyo kuimba kwenye kwaya ya Flying Family haimaanishi kuacha kuhudumu kwenye kwaya za kanisa anakotokea mwanakwaya,” anasema

Aidha anasema sehemu kubwa ya mazoezi yanafanyika kwa njia ya mtandao wa WhatsApp ambapo kila sauti ina kundi lake na walimu wa kuwasimamia siku zote za wiki na jumapili inakuwa ni siku ya kuunganisha tu.

“Mwalimu anajirekodi na kuwatumia, kisha kila mwanakwaya anasikiliza na kujifunza na kisha kujirekodi na kutuma tena kwenye group kwa ajili ya mwalimu kusikiliza na kurekebisha. Kwa sasa tumeenda mbali zaidi ambapo nyimbo nyingi wanakwaya wanasikiliza wao wenyewe kupitia mtandao wa Youtube.

“Kisha mwalimu wa kila sauti hukutana na kundi lake kwa ajili ya masahihisho kabla ya kwaya nzima kukutana na kuunganisha siku ya jumapili. Kwaya ina walimu kumi na moja wenye uwezo mkubwa wa kusoma muziki, kupiga kinanda na piano, utunzi wa kiwango cha juu kabisa pamoja kufundisha somo la muziki kwa wanakwaya na wasio wanakwaya,” anasema Fundisha

Anasema yote hayo yanafanyika chini ya kikosi imara cha wataalamu kikiongozwa na Mwalimu Wakili Nereus Mutongore, CPA Innocent Fundisha, Egidius Mushumbusi, Jerry Newman, Eng. Deogratias Ngereza, Mathias Msafiri, Ainamringi Foya, Eng Pauline Tumaini, Lucy Mutongore, Elizabeth Malenga na Eng. Patrick Mamsery.

Matarajio ya kikundi

Fundisha anasema matarajio ya kwaya hiyo ni kutambulika na kuheshimika kimataifa kupitia kiwango cha juu kabisa cha ubora wa muziki na matamasha yake na kwamba hayo yote yatatokana na mipango sahihi ya kujutuma na nidhamu ya hali ya juu katika kuishi malengo ya kwaya.

Wito kwa watu wengine

Anasema wanawashauri vijana kutumia muda na vipaji vyao kumtukuza Mungu kwani ndiye aliyewapa vyote walivyo navyo.

Fundisha anasema kupitia vikundi vya uimbaji wanamtukuza Mungu na kupata wasaa wa kuepuka kushiriki vitendo viovu huko mitaani hivyo upata baraka na neema kwa kufanya yampendezayo Mungu.

“Tunatoa wito kwa wakristo wote kutambua kuwa sisi sote ni kondoo na mchungaji wetu ni mmoja Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo yatupasa kuishi kwa umoja na mshikamano na inawezekana kushirikiana bila kujali tofauti zetu za kimadhehebu.

“Lakini pia tunatoa wito kwa wenye vipaji vya kuimba au kupiga vyombo vya muziki wajiunge nasi kwa kufuata taratibu watakazopewa ili kudumisha umoja huu na kuueneza kwa wengi zaidi,” anasema

Hata hivyo anasema wanawashukuru wadau mbalimbali hasa walezi wao ambao ni maaskofu, wachungaji, mapadre pamoja na waamini kwa kuwapa moyo, kuwaongoza na kuwashauri, kuwawezesha kwa hali na mali bila kuwasahau watu binafsi na taasisi kama Paones General trading ambao wanawafadhili kwenye matamasha yao.

Aidha anatoa wito kwa wote wenye mapenzi mema kuendelea kuchangia kazi hii kupitia MPESA lipa namba 5226676 au NMB akaunti namba 22510097145 au kuwasiliana nao kwa namba 0764 088 006

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here