Chato
HUDUMA za matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) katika hospitali ya rufaa ya kanda Chato zimezinduliwa rasmi.
Huduma hizo zimezinduliwa leo Novemba 6, 2024 na Katibu Tawala Mkoa (RAS) Geita Mohamed Gombati katika hospitali ya rufaa ya kanda Chato .
RAS Gimbati amesema dhumuni la MOI kusogeza huduma za kibingwa na bingwa bobezi ni kumpunguzia mwananchi gharama ya kusafiri hadi jijini Dare es Salaam kufuata huduma hizo.
“Nimefurahi kusikia kuwa hospitali yetu imeingia makubaliano ya ushirikiano ya utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi za Taasisi ya MOI, makubaliano haya siyo tu yatasogeza huduma kwa wananchi lakini pia yatawapunguzia gharama na adha kubwa wagonjwa waliolazimika kufuata huduma hizi MOI, Dar es Salaam,”amesema.
Amesema makubaliano hayo ni ishara ya kuyaishi matarajio na matamanio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Haasan ya kuhakikisha wananchi anapata huduma za kibingwa na kibobezi karibu na maeneo yao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya rufaa ya kanda Chato Dk. Oswald Lyapa amesema lengo la ushirikiano huo na Taasisi ya MOI ni kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu karibu na wananchi wa kanda ya ziwa.
Daktari bingwa na mbobezi wa mifupa kutoka MOI Dk. Bryson Mcharo amesema MOI kwa siku mbili wamewahidumia wagonjwa ambao kweli walikuwa wanahitaji huduma za kibingwa na bobezi za MOI hivyo amewataka wakazi wa kanda ya ziwa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi hospitali hapo kupata matibabu.