Arusha
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wasimamizi wote wa rasilimaliwatu wazingatie misingi ya utawala bora na weledi katika kuisimamia rasilimali hiyo katika Sekta ya Umma Barani Afrika.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha kutoa huduma bora na kudumisha imani ya wananchi kwa Serikali zao.
Ametoa wito huo leo Jumatatu, Novemba 4, 2024 alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Mwaka wa Mtandao wa Wasimamizi na Mameneja wa Rasilimaliwatu Katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMnet) jijini Arusha.
“Rasilimaliwatu ina mchango mkubwa katika kuiwezesha Serikali kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Hivyo ninyi, kwa kuwa ni wataalam katika usimamizi wa Rasilimaliwatu mnao wajibu na dhamana kubwa ya kuhakikisha mnasimamia ipasavyo Rasilimali hiyo muhimu na ya thamani,”amesema .
Amesema kuwa ili kuimarisha usimamizi wa kimkakati wa rasilimaliwatu na kukabiliana na changamoto zake, viongozi hao wanapaswa kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wao waendane na mabadiliko ya kidunia na waweze kufanya kazi kwa weledi.
Aidha, amewataka Kukuza ujuzi wa watumishi na kuwawezesha kujifunza stadi mpya kulingana na majukumu yao. “Ongozeni kwa maono, ubunifu, uadilifu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi husika katika kutumikia wananchi kwenye maeneo yenu”
Majaliwa amewataka viongozi hao kutafsiri kwa vitendo Dira ya APS-HRMnet ya kuunda mtandao thabiti wa kitaalamu wa mameneja wa rasilimaliwatu katika sekta ya umma kwa kufanikisha malengo ya huduma bora.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema kuwa mkutano huo umefanyika katika kipindi ambacho dunia ina changamoto zinazohitaji mijadala, kubadilishana mawazo ili kujibu masuala magumu yanayosababisha watumishi wa umma kutofanya majukumu yao sawasawa.
Naye, Rais wa Mtandao huo Xavier Mrope Daudi amesema kuwa lengo lao ni kukuza ubora, uadilifu na viwango vya taaluma katika utendaji wa usimamizi wa rasilimali watu kwenye sekta ya umma barani Afrika.
“Pia lengo jingine ni kutambua na kushirikisha mbinu bora katika usimamizi wa rasilimali watu ili kusaidia sekta ya umma kuboresha utendaji kazi katika usimamizi wa rasilimali watu.
Kaulimbinu ya mkutano huo ni “Utawala stahimilivu na Ubunifu: Kukuza Sekta ya Umma ijayo kupitia Uongozi wa Rasilimaliwatu”