Home KITAIFA WANANCHI WAPEWA TAHADHARI YA KUTOKUSOGELEA GARI LILOBEBA KEMIKALI YA SIANDI LINAPOPATA AJALI

WANANCHI WAPEWA TAHADHARI YA KUTOKUSOGELEA GARI LILOBEBA KEMIKALI YA SIANDI LINAPOPATA AJALI

Dar es Salaam

WANANCHI wametakiwa kutolisogelea gari lililobeba kemikali ya siandi (Sodium Cyanide) pindi linapopata ajali badala yake wachukue tahadhari kwa kukaa umbali wa mita 100 ili kutopata madhara mbalimbali ikiwemo ya kupoteza maisha pindi wakivuta hewa yenye sumu inayotokana na kemikali hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Novemba, 4 2024 jijini Dar es Salaam na Mkemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Derick Masako wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa elimu kwa umma juu kemikali hiyo ambayo inatumika katika kuchenjua dhahabu migodini.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa maeneo ya Mbezi mwisho inaendeshwa na kampuni ya usafirishaji wa kemikali ya Taifa Transport and Logistic Limited, Kampuni ya Freight Forwarders Tanzania, Mainline Carriers pamoja na Swala Solution Limited.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, Masako amesema kemikali hiyo ya Siandi imeanza kuingia nchini tangu mwaka 1990 na toka wakati huo hadi leo imekuwa ikisafirishwa bila kuleta madhara yoyote kwa binadamu.

Amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali chini ya mamlaka ya GCLA bado wanaendelea kuwasisitiza wananchi kutosogelea magari yanayobeba kemikali ikiwemo ya sianidi pindi yanapopata ajali.

“Ajali za kemikali hii ziliwahi kutokea mbili moja gari lilipinduka katika mkoa wa Singida na nyingine kontena lilianguka mkoa wa Shinyanga, lakini kutokana na kwamba wale wasafirishaji walikuwa na elimu waliweza kuwazuia wananchi wasisogee eneo la tukio.

“Kemikali hii ikimwagika na kuchanganyika na maji inaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu kwani inatoa hewa chafu ya sumu ambayo mtu akiivuta inaweza kumsababishia kifo kwa haraka,” amesema Masako

Baadhi ya magari yaliyobeba kemikali ya Sianidi

Aidha amesema kampeni hiyo ni mahususi kwa ajili ya watu wanaoishi pembezoni mwa barabara kuanzia Dar es Salaam kwenda katika mikoa amabyo inatumia kemikali hiyo ambayo ni Geita, Shinyanga na Mara.

Amesisitiza kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali anasimamia sheria tatu ambazo ni usimamizi wa kemikali za viwandani na majumbani, sheria ya usimamizi wa taarifa za vinasaba za binadamu na mwisho ni ile inayohusu mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali.

“Mbali ya sheria hizo Mkemia Mkuu wa Serikali anasimamia kituo cha udhibiti wa matukio ya sumu. hivyo mamlaka inajukumu la kuwasisitizia wadau wanaosafirisha kemikali hizi kuendelea kutoa elimu kwa jamii, hata hivyo Kemikali hii ya sianidi ndiyo inayotoa dhahabu kwenye miamba,” amesema

Ofisa Usalama Mahala pa Kazi kampuni ya Taifa Transport and Logistic Limited, Bestina Kitinya akitoa elimu kwa wananchi (hawapo pichani) kuhusiana na kemikali ya sianidi.

Naye Ofisa Usalama Mahala pa Kazi kampuni ya Taifa Transport and Logistic Limited, Bestina Kitinya amesema hatua ya kwanza ya kujikinga na kemikali hiyo pindi ikimwagika barabarani basi watu watakaokuwepo eneo hilo watapaswa kuvaa barakoa na kukimbia umbali wa mita 100.

“Na unapokimbia hakikisha unakimbia kwa kuangalia upepo unapotokea, pia ikitokea mtu amemgusa yule ambaye ameathirika na kemikali hiyo ya Sianidi mfano dereva aliyekuwa akiendesha gari bila kujikinga anaweza kupata madhara pia, hivyo unapaswa kutomgusa sehemu zenye jasho,” amesema

Mratibu wa Usalama, Afya na Mazingira kutoka Kampuni ya usafirishaji ya Freight Forwarders Tanzania, Sadiki Yusufu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji elimu kwa jamii kuhusu kemikali ya sianidi

Kwa upande wake Mratibu wa Usalama, Afya na Mazingira kutoka Kampuni ya usafirishaji ya Freight Forwarders Tanzania, Sadiki Yusufu amesema elimu hiyo ni muhimu kwa jamii kwani kemikali hiyo ni muhimu katika sekta ya uchimbaji dhahabu duniani kwani ina uwezo mkubwa wa kuondoa dhahabu kwenye mwamba.

Amesema wakati wanasheherekea mafanikio ya kemikali hiyo, wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha jamii ya watanzania inataarifa za msingi juu ya kemikali ya sianidi hususani wale ambao wanafanya shughuli zao kandokando ya barabara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here