Dar es Salaam
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amewakumbusha wake wa marais Afrika kuwa wananafasi muhimu katika jamii, wachukue suala la nishati safi ya kupikia kwa hekima na kwa ushawishi mkubwa marais waichukue kama ajenda yao.
Pia amewataka waendelee kutoa ushauri wa hekima katika kuangalia namna ya kuweka vipaumbele vya afua vitakavyosaidia kuwawezesha wanawake na kuboresha ustawi wao.
Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba, 29 jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa 11 wa taasisi ya Merck Foundation na kuhudhuriwa na baadhi ya wake wa marais kutoka nchi 15 za Afrika na washiriki zaidi ya 400.
“Nimekuwa nikitumia nafasi yangu kuonesha mitazamo inayokosekana na kutoa mapendekezo ambayo yataweza kushughulikia masuala ya wanawake.
“Nimekuwa nikishughulikia suala la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Afrika ikiwa sehemu ya kuongeza usawa wa kijinsia katika kutumia nishati safi na kuachana na mkaa na kuni ambayo inaathiri afya za wanawake na ustawi wao na kuharibu mazingira,” amesema.
Rais Dk. Samia amesema amekuwa akitumia nafasi yake ya Rais katika kuonesha mitazamo iliyokosekana na kutoa mapendekezo kwa lengo la kumkomboa mwanamke.
Alisema katika wamepokea msaada mkubwa wa kutekeleza mpango huo ambao utawezesha wanawake na kuboresha ustawi wao katika bara zima la Afrika.
“Nimefanya yote hayo kama Rais lakini leo niwakumbushe wake za marais kuwa mnayo nafasi muhimu katika jamii zenu, chukueni suala la nishati safi ya kupikia kwa hekima na kuwa na ushawishi mkubwa marais waichukue hiyo kama ajenda yao na kuwasaidia wanawake kutumia nishati safi ya kupikia,”amesema.
Amewapongeza kwa kuwa na program za kufikia malengo ya hatma ya kuwa na watu wenye afya bora hasa wasichana na waanawake Afrika hivyo aliwataka waendelee kutoa ushauri kwa hekima katika kuangalia namna ya kuweka vipaumbele vya afua vitakavyosaidia wanawake na kuboresha ustawi wao katika nchi zao.
Rais Dk. Samia amesema Tanzania inayodhamira ya kuendelea kushirikiana na washirika waliopo nchini kufikia hatma yenye afya na furaha zaidi kwa vizazi vijavyo.
Amesema Tanzania inayofahari kubwa kushirikiana na taasisi hiyo kwani kwa miaka michache wameshuhudia maendeleo makubwa hususani kwa sekta ya afya.
“Tunathamini sana ushirikiano huu, umetuwezesha Watanzania kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu ya ubobezi katika afya ni mategemeo yetu tutakuza ushirikiano huu katika miaka ijayo,” amesema.
Amesema miaka tisa iliyopita Umoja wa Mataifa uliopitisha malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs, miongoni mwa malengo hayo ni kuhakikisha kunakuwepo na elimu jumuishi, kuimarisha nyenzo za utekelezaji wa ushirikiano wa kidunia kwa maendeleo endelevu.
Ameipongeza kongamano hilo la 11 kwani limekuja wakati muafaka ikiwa ni kipindi cha utekelezaji wa taarifa za maendeleo endelevu hususani kwa sekta ya afya na elimu.
Amesema wanapokwenda kutekeleza malengo hayo, majadiliano yanayotakiwa kufanyika katika kongamano hilo ni muhimu kwani lazima wawe makini na ushirika wa pamoja huku Tanzania ikiahidi kuchangia kwa kiasi kikubwa.
SEKTA YA AFYA
Akizumgumza katika mkutano huo, Rais Dk. Samia amesema serikali yake imetoa kipaumbele kikubwa katika kuboresha afya mama na mtoto kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga hospitali za wilaya 127 na vituo vya afya 300.
“Tuliongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vinatoa huduma za uzazi na mtoto kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi 523, mwaka 2023, kupunguza vifo vya uzazi mwaka 2021 kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 104 ikiwa punguzo la zaidi ya asilimia 80,” amesema.
Rais Dk. Samia amesema vifo vya watoto vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000 sawa na theluthi moja.
Amesema kuna hatua zaidi za kufanya kufikia malengo ya afya ya mama na mtoto kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za kibobezi kwa sababu moja ya changamoto wanayokumbana nayo ni upungufu wa wataalamu bobezi na wenye ujuzi.
Ameishukuru taasisi ya Merck kwa kutoa elimu kwa madaktari wa kitanzania hususani kwa huduma za kibobezi hivyo aliahidi kuendelea kushirikiana nao kuzalisha idadi kubwa ya huduma za kibobezi nchini.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima amesema mkutano huo ni wa kwanza kihistoria kufanyika nchini.
Ametaja vitu vilivyochangia mkutano huo kufanyika nchini ni ushirikiano wa Rais Dk. Samia na taasisi ya Merck katika jitihada za kukabiliana na matatizo na changamoto za kiafya na kijamii zinazoathiri jamii zetu hususani wanawake na wasichana.
“ Kwa siku mbili tutashiriki mijadala ya kisayansi inayofanywa na wataalamu bobevu watakoonesha jitihada na kazi zao katika kupambana na magonjwa kama vile afya ya uzazi, sukari na aina mbalimbali za saratani ambazo huathiri wanawake kwa kiwango kikubwa,”amesema.
Dk.Gwajima amesema jamii kuelewa kukabiliana na changamoto hizo ni muhimu hasa wanapoendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na mijadala itakayowasilishwa haitashughulikia matatizo ya afya tu bali itahusu ku boresha maisha na kuunda mustakabali endelevu kwa jamii.
Amesema Tanzania imeweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi ya Merck, Profesa Frank Haverkamp amesema taasisi hiyo imejikita katika kuboresha Afya na ustawi katika huduma za afya eneo la Afrika, Asia na kwingineko.
Amesema katika kufanikisha jambo hilo, wamekuwa wakitoa udhamini wa masomo katika kada ya afya kwa ngazi tofauti na kutoa semina kuhusu afya bora na ustawi wa afya.