Home KITAIFA SAMIA KALAMU AWARD YASOGEZA MBELE MUDA WA KUWASILISHA KAZI KUSHIRIKI TUZO ZA...

SAMIA KALAMU AWARD YASOGEZA MBELE MUDA WA KUWASILISHA KAZI KUSHIRIKI TUZO ZA HABARI ZA MAENDELEO

Dar es Salaam

CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameongeza muda wa maombi ya ushiriki katika Tuzo za Samia Kalamu Awards hadi Oktoba 30, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 24, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Dk. Rose Reuben amesema awali tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ilikuwa Oktoba 26, mwaka huu.

“Tunapenda kuwataarifu waandishi wa habari, vyombo vya habari, maafisa habari na wadau wa habari kuwa muda wa kuomba kushiriki katika tuzo umesogezwa mbele hadi Octoba 30,2024,”alisema.

Amesema uamuzi wa kuongeza muda umechukuliwa ili kutoa nafasi kwa wale waliokutana na chagamoto za kiufundi, ikiwemo kushindwa kuipandisha kazi mtandaoni kutokana na matatizo ya mtandao na chagamoto nyingine.

Amesema Tuzo hizo zitatolewa kwa wanahabari wa kitanzania zikiwa na lengo la kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani, kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni, ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo.

Aidha amewaomba wale wote ambao awajawasilisha kazi zak kuchukua hatua za haraka na kufanya hivyo kabla kufikia Octoba 30, 2024 .

“Hii ni fursa adhimu kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari, maafisa habari kuonesha umahiri wao wa kuchakata habari na kuthaminiwa Kwa michango yao katika taaluma ya uandishi,”amesema.

Amesisitiza kuwa kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine, na zinazofuata taratibu za haki miliki. Waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti rasmi ya www.samiaawards.tz

Akizungumzia kuhusu takwimu za maombi ya tuzo Dk. Rose alisema hadi Oktoba 23, mwaka huu wamepokea maombi kutoka mikoa 23 ya Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Simiyu, Geita, Njombe, Mbeya, Songwe,Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Mjini Magharibi, Ruvuma, Lindi, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro na Pwani.

Pia amesema mchakato wa upigaji kura Kwa wananchi inatarajia kuanza rasmi Novemba 8 mwaka huu hivyo aliwahimiza wanahabari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhim wa kushiriki katika upigaji kura kwa wingi, kwani kura za wananchi zinachangia asilimia 60 ya alama za mshindi, huku asilimia 40 zikiamuliwa na jopo la majaji.

Ameongeza kuwa wananchi wataweza kupiga kura kupitia namba maalumu ya SMS SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi.

Kwa upande wake Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA,Mhandisi Andrew Kisaka amesema tuzo hizo ni muhimu kwa ajili ya kukuza na kutambua mchango wa waandishi wa habari katika masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo.

“Nawahimiza wanahabari kutoka redioni, televisheni na mitandao ya kijamii kuziwasilisha kwa haraka katika kipindi hiki kilichobaki kwani tunaamini zimeleta mabadiliko chanya kwenye jamii,”amesema Mhandisi Kisaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here