Atembelea na kukagua Mradi wa Gesi ya Hellium uliyo katika hatua za utafiti
Rukwa.
NAIBU Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, amewataka wananchi wa mkoa wa Rukwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kuomba Leseni za Uchimbaji Mdogo ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.
Dk. Kiruswa ametoa wito huo Oktoba 24, 2024, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Zimba na Misheni vilivyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya Sekta ya Madini mkoani humo.
Amesema kuwa, kutokana na utajiri wa rasilimali za madini zilizopo mkoani Rukwa, ni wakati wa wananchi kuchangamkia fursa za kushiriki katika mnyororo wa shughuli za madini ikiwemo kuchimba na kwa Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kunufaika moja kwa moja na rasilimali hizo.
“Lengo kuu la Serikali yetu ni kuona kwamba rasilimali zilizopo zinawanufaisha wananchi wa Rukwa na taifa kwa ujumla, na njia bora ya kufanikisha hilo ni kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hizi kwa kuomba leseni za uchimbaji mdogo, nendeni katika Ofisi za Madini za Mkoa mtapewa utaratibu wa kufuata na mtapewa elimu pia kuhusu namna ya kundesha shughuli zenu kwa kufuata Sheria na Kanuni zinazotuongoza,” amesema Dk. Kiruswa.
Ameongeza kuwa kwa kuhakikisha wananchi wanapata leseni na kushiriki katika uchimbaji wa madini, uchumi wa mkoa wa Rukwa utaimarika zaidi, huku ajira zikiongezeka na kipato cha wananchi kuimarika.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amewataka wawekezaji wa kampuni ya Noble Helium, ambao wanaendesha mradi mkubwa wa uchimbaji wa gesi ya helium katika mkoa wa Rukwa na hivi sasa wakiwa katika hatua za utafiti, kuhakikisha wanaweka uhusiano mzuri na wakazi wa maeneo yanayozunguka mradi wao na kuwataka wawekezaji hao kujenga mahusiano ya ushirikiano na jamii, kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wanaona na kunufaika na uwepo wa mradi huo katika eneo lao.
Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Noble Hellium, Edwin Mremi amemhakikishia Naibu Waziri Kiruswa kuwa Kampuni hiyo inawajibika kutengeneza uhusiano mzuri na jamii inayozunguka mradi huo na kwamba tayari wametoa vipaombele kwa ajira kwa wakazi wa maeneo hayo wakati huu Kampuni ikiendelea na utafiti.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu ameeleza kuwa ukubwa wa eneo lilifanyiwa utafiti wa awali na kuonesha kuwa na rasilimali ya madini linatosha kugawa leseni 718 kwa wachimbaji wadogo mkoani humo, huku akiwakaribisha kuchangamkia fursa za uchimbaji mdogo.