Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha Tanzania (TAMFI) lilifanya mkutano maalum wa ushawishi (Advocacy) na wadau mbalimbali Oktoba, 4 2024 jijini Dar es Salaam.
Pia Mkutano huo lulilenga kujadili maendeleo ya sekta kwa ujumla na kutathmini mchango wa sekta hiyo katika Uchumi wa taifa. Aidha mkutano ulijadili namna ya kuongeza ufanisi wa huduma ili kuboresha taswira ya sekta ya huduma ndogo za fedha katika jamii.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAMFI, Devotha Minzi, alibainisha kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi ndogo za fedha, hasusani wateja wa TAMFI katika kuwafikishia mikopo wananchi ambao bado hawajaweza kufikiwa na taasisi kubwa za fedha yakiwemo mabenki.
Ametoa msisitizo juu ya hilo, mwenyekiti alieleza kuwa ongezeko la kiasi cha mikopo kinachotolewa na wanachama wa taasisi ndogo za fedha ni uthibitisho wa uhitaji mkubwa wa mikopo uliopo nchini.
Ikumbukwe kuwa taasisi ndogo za fedha zinawakopesha wateja ambao ni hatarishi zaidi kiuchumi kwa wengi kukosa baadhi ya vigezo vya kukopesheka vinavyohitajika na taasisi kubwa za fedha.
Sekta hii, inaendelea kuwa sehemu mhimu sana katika kupanua wigo wa fedha (financial Inclusion) hasa kwa mikopo inayoenda katika Nyanza ya uzalishaji na ujasiriamali.
Hata hivyo, mwenyekiti amesisitiza kuwa Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na wanachama wengi wa TAMFI ambao wanafuata taratibu bora za ukopeshaji, ni mhimu kikao hiki kikajadili, kutathmini na kutafuta suluhu juu ya malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wateja wetu ili kuongeza ufanisi wa huduma zetu na kujenga taswira nzuri kwa jamii.
Malamiko juu ya gharama kubwa za ukopeshwaji pamoja na kutofuata taratibu bora za ukopeshaji ni moja ya maswala ambayo yanapaswa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Amesema pamoja na kutathmini mchango mkubwa wa sekta yetu katika uchumi mpana na uongezaji wa wigo wa fedha katika jamii, tutathmni maeneo yanayohitaji maboresho katika utoaji wetu wa huduma ili kuongeza ufanisi na kujenga taswira nzuri katika jamii.
Katika kuboresha huduma, mkutano utashuhudia uwasilisha wa Kanuni za Maadili ya Uendeshaji Huduma (CODE OF CONDUCT), Lengo lao ni wanachama wa TAMFI kujitofautisha na wakopeshaji wengine kupitia maadili bora tuliyokubaliana.
Kupitia mkutano huu, wanachama watatakiwa kutoa mapendekezo ya jinsi TAMFI inaweza kusaidia katika kuimarisha tasnia endelevu ya huduma hizo.
Miongoni mwa masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa ufuatiliaji wa miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kuhakikisha kuwa taasisi zote zinazotoa huduma ndogo za fedha zinafuata sheria na taratibu ili kudumisha uwazi na uwajibikaji.
Aidha, Devotha amesisitiza kwamba TAMFI inaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma na wateja wao ili kuhakikisha kuwa sekta hii inaendelea kukuza uchumi wa jamii na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kifedha nchini.
Katika mkutano huo, washiriki walipata fursa ya kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya utoaji huduma ndogo za fedha na kubaini njia za kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma.
“Shutuma zimekuwa nyingi, zikituita majina kama ‘kausha damu’, na mengine ambayo si sahihi, mara nyingi shutuma hizo zimeangalia upande mmoja wa mkopaji bila kumsikiliza mkopeshaji. Kama watoa huduma, tungependa kutoa huduma bora iliyo endelevu na isiyomuumiza mteja. Lengo letu ni kutoa huduma inayolenga kumsaidia mteja, na siyo kumuumiza.
Kama tulivyosikia kutoka kwa mashuhuda ambao ni wateja wa taasisi ndogo za fedha, Tumesikia wateja kadhaa wakieleza jinsi walivyofaidika na mikopo waliopata kutoka katika zetu. Wameeleza jinsi walivyokopa mara nyingi na kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi. Wengi wanaotuita majina hayo mabaya ni wale ambao kwa sababu mbali mbali wameshindwa kurejesha mikopo yao ikiwemo wengine kukimbia na mkopo bila taarifa. Lengo letu ni kutoa mkopo utakaokuwa na tija kwa wateja wetu na sio vinginenvo ” alisema Devotha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMFI, Winnie Terry, ameeleza kuwa sekta ya microfinance ina fursa nyingi sokoni, ingawa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazozikumba taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha.
Amesisitiza kuwa taasisi hizi zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya taifa, kwani zinatoa huduma zinazohitajika kwa kiasi kikubwa na wananchi wengi ambao hawapati huduma za kifedha kwa urahisi kupitia mifumo rasmi ya kibenki.
Terry, ameeleza kuwa TAMFI inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza uwazi na ufanisi wa sekta ya huduma ndogo za fedha, huku akiwataka wadau wote kuendelea kushirikiana na kuzingatia maadili ili kuboresha tasnia nzima na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Tumeweka mikakati ya namna ya kukabiliana na changamoto hizi ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora. Tunaangalia pia maadili ya kazi na kuhakikisha wanachama wetu wanafuata misingi ya maadili tuliyokubaliana. ,” amesema Winnie.
Ameeleza kuwa TAMFI ni muungano wa taasisi zinazotoa mikopo, akiba, na huduma nyingine za kifedha, na malengo yake makuu ni kukuza upatikanaji wa huduma za fedha, kuboresha ufanisi wa huduma hizo, na kulinda maslahi ya wateja. Shirikisho hili lilianzishwa mwaka 2011 na limeendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya sekta ya huduma ndogo za fedha nchini.
Pia ametoa wito kwa wadau wengine kujiunga na TAMFI ili wapate fursa ya kushiriki mijadala na kuchangia katika ukuaji wa sekta hiyo.
Naye Muhasibu wa BK Finance Limited, Roymez Kway, alisema kushiriki kikao hicho ni fursa kwa sababu kimetoa mwongozo wa kuimarisha ushirikiano na kuleta taswira ya pamoja kwa watoa huduma ndogo za fedha na hivyo kuboresha huduma kwa wateja wao.
Warsha hiyo ilihitimishwa kwa ahadi thabiti kutoka kwa watoa huduma ndogo za fedha kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Watoa huduma walisema ni muhimu kuwa na ushirikiano wa kweli kati ya wadau wote, wakiwemo watoa huduma, wakopeshwaji, na serikali, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wateja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi mbalimbali kutoka taasisi muhimu zinazojihusisha na huduma ndogo za kifedha na huduma za kifedha kwa ujumla. Washiriki walijumuisha maafisa mawasiliano na fedha, Wakurugenzi Wakuu, Wakurugenzi, na Mameneja kutoka mashirika mbalimbali kama vile BRAC Tanzania Finance, SELF Microfinance, Endeleza Credit, na mengineyo.
Ushiriki wao ulionyesha dhamira ya dhati ya kuendeleza majadiliano kuhusu hali ya sasa ya huduma ndogo za kifedha nchini Tanzania na kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili watoa huduma na wakopaji.
Warsha hiyo imetoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kushughulikia masuala ya sekta, na kuchunguza mikakati ya kuboresha upatikanaji na athari za huduma za kifedha kwa jamii ambazo hazifikiwi kwa urahisi na huduma hizo.