Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya watanzania 31,282,331 wamejiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024, ambao ni sawa na asilimia 94.83 ya lengo la kuandikisha wapiga kura 32,987,579.
Waziri Mchengerwa ametoa takwimu hiyo ya watanzania waliojiandikisha kupiga kura, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TAMISEMI.
“Watanzania wanaume waliojiandikisha ni 15,236,772 sawa na asilimia 48.71 na wanawake ni 16,045,559 sawa na asilimia 51.29 ambao kwa mujibu wa kanuni na sharia ndio watashiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu,” ameainisha Mchengerwa.
Amesema, takwimu zinaonesha kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 ambapo waliandikishwa wapiga kura 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.
Ameeleza kuwa, ongezeko la idadi ya wapiga kura limetokana na jitihada za uelimishaji na uhamasishaji katika ngazi zote za muhimu zilizofanywa na Ofisi Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, Mchengerwa amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, tasasi za kiraia, wasanii, vyama vya siasa na wadau wengine kwa kuwahamasisha na kuwaelimisha watanzania wenye sifa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha.
“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji, orodha ya wapiga kura inabandikwa kuanzia leo katika sehemu za matangazo ya uchaguzi kwenye vijiji na mitaa ili kuwawezesha wananchi kukagua orodha hiyo na kufanya marekebisho iwapo itabainika kuna mapungufu,” amesisitiza Mchengerwa.
Amefafanua kuwa, ukaguzi huo utafanyika kwa muda wa siku 7 kuanzia leo tarehe 21 hadi 27 Oktoba, 2024 hivyo ametoa wito kwa wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza ili kuhakiki orodha hiyo itakayobandikwa katika vijiji na mitaa wanayoishi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu utafanyika Novemba 27, ambapo jumla ya watanzania 31,282,331 waliojiandikisha ndio wenye haki ya kikatiba ya kushiriki uchaguzi huo kwa kuchagua wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa, wajumbe wa halmashauri ya kijiji pamoja na kamati ya mtaa.