Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelikabidhi Jeshi la Polisi magari 77 kwa ajili kurahisha utekelezaji wa majukumu yake ya kusimamia usalama wa raia na mali zao ikiwa ni mwendelezo jitihada za Serikali kulifanya Jeshi hilo kuwa la kisasa lenye vifaa, na weledi wa kuzuia uhalifu.
Akikabidhi magari hayo leo Oktoba 19 2024 kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Waziri Masauni amelitaka Jeshi hilo kuhakikisha kuwa linayatumia vyema magari hayo kwa kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi ikiwa ni sambamba na kuyatunza ili kuthamini jitihada za Serikali kuliboresha Jeshi hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP. Camillus Wambura ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi hilo kuwa la kisasa hivyo ni wajibu Polisi kuhakikisha uhalifu unaendelea kupungua huku akiwaasa madereva wa magari hayo kuzingatia sheria za usalama barabarani ili magari hayo yaweze kudumu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa ametoa rai kwa madereva wa magari hayo kupatiwa mafunzo huku Mkurugenzi wa Kampuni ya Kifaru Motors, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo akiahidi kuwa kampuni yake imejiandaa kulisaidia Jeshi hilo msaada kitaalamu, ushauri na kiufundi pale itakapohitajika.