Home KITAIFA SERIKALI YAANZA KUTOA VITAMBULISHO VYA KISASA KWA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO

SERIKALI YAANZA KUTOA VITAMBULISHO VYA KISASA KWA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO

Arusha

SERIKALI imezindua rasmi ugawaji wa vitambulisho vya kidijitali kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo nchini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima akizungumza na wafanyabiashara hao na wananchi wa jijini Arusha wakati akizindua vitambulisho hivyo leo Oktoba 17, 2024, amebainisha kuwa vitambulisho vitakuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara ndogondogo kuwainua kiuchumi.

Amesema Serikali kwa vipindi tofauti imeendelea kushughulikia changamoto za wafanyabiashara ndogondogo na kwa kutambua juhudi hizo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendeleza juhudi hizo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa uchumi jumuishi.

Dk. Gwajima amezitaja baadhi ya juhudi hizo ni pamoja na ujenzi wa ofisi za wafanyabiashara ndogondogo na kuwapanga kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa na Serikali ambapo hadi sasa mikoa kumi na mbili (12) imekamilisha ujenzi wa ofisi hizo.

Ametaja pia uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, uratibu wa utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo ambapo Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zimeendelea na jitihada za kuwaendeleza kiuchumi ikiwemo mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri na mikopo kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi na Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Kwa upande wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeingia mkataba na Benki ya NMB wenye thamani ya Shillingi Bilioni 18.5 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara hao. Vilevile Wizara itaendelea kutumia mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) kuwezesha wanawake wajasiliamali.” amesisitiza Dk. Gwajima.

Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda akizungumza katika tukio hilo, ametoa wito kwa wafanyabiashara ndogondogo kutumia fursa hiyo ya pekee kwao ili kujinufaisha zaidi kiuchumi huku akiwahimiza wananchi wote kushirikiana kutokomeza vitendo vya ukatili kwa kutoa taarifa za ukatili wa namna mbalimbali mkoani humo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Seif Shekalaghe, akieleza umuhimu wa vitambulisho hivyo, amesema baada ya mfumo huu kukamilika mkoa wa Arusha umeongoza katika kujisajili na kulipia kwa wingi vitambulisho hivyo vya kidijitali vitakavyowawezesha kupata mkopo na huduma nyingine za kifedha.

Shekalaghe ameeleza faida nyingine ni pamoja na kuunganishwa na mifumo ya kibenki, mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kadri Serikali na mfanyabiashara ndogondogo watakavyokubaliana ili wanufaike na fursa za mikopo yenye masharti nafuu kupitia taasisi za fedha na kuweza kuweka akiba ya uzeeni kwa kadri atakavyokuwa anachangia kwenye mifuko hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara ndogondogo nchini, Katibu wa shirikisho la Umoja wa Machinga SHIUMA, Venatusi Magayane ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi yao na kutatua changamoto zao, ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana kwa maslahi mapana ya wafanyabiashara ndogondogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here