Arusha.
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini limewataka madereva kufuata sheria za Usalama Barabarani ambapo limewataka madereva hao kutoa lugha nzuri na rafiki kwa abiria Pamoja na kuongea nao kabla ya safari kuanza huku likiwapiga faini madereva ambao hawana sanduku la dhalula.
Akizungumza leo Alfajiri Oktoba 16,2024 Katika kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi Jirani jijini Arusha Mkuu wa kitengo cha Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya kikosi cha Usalama Barabarani Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Michael Deleli amewaonya na kuwataka madereva kutumia lugha nzuri kwa abiria wanaowahudumia.
Ameongeza kuwa endapo dereva hatopata shukrani kutoka kwa abiria atambue kuwa ajatoa huduma nzuri kwa abaria wake ambapo amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani na kutoa huduma nzuri ili abiria waridhike na huduma wanazotoa kila mara.
ACP Deleli amesisitiza suala la kuongea na abiria kabla ya safari ili kutambua changamoto za abiria wao huku akiwataka kutumia lugha nzuri amabazo wanazitoa kwa wateja wao kabla na wakati wote wa safari.
Naye Domisiano Msakalile ambaye ni miongoni mwa abiria wanatumia vyombo hivyo licha ya kushukuru kikosi cha usalama barabarani nchini kwa kuendelea kutoa elimu kwa madereva na abiria amebainisha kuwa elimu hiyo imemuongezea maarifa na utambuzi wa mambo na haki zake kama abiria anayetumia vyombo hivyo.
Kwa upande wa madereva wanaofanya safari zao kutoka Mkoani Arusha Kwenda mikoa mbalimbali na nchi Jirani pamoja na kushukuru kikosi cha usalama Barabarani kwa kutoa elimu wakawaangushia lawama abiria ambao wamekuwa wakiwalazimisha kushuka na kupata huduma mbalimbali za kijamii maeneo yasio ruhusiwa kupata huduma husika.