Home KITAIFA DK. MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA KAZILAMBWA-CHAGU (KM 36)

DK. MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA KAZILAMBWA-CHAGU (KM 36)

Tabora

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi Barabara ya Kazilambwa- Chagu na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuzilinda Barabara na alama za Barabarani ili kuepuka ajali.

Akizungumza na wananchi wa Ugansa wilayani Kaliua, mkoani Tabora, Oktoba 11, 2024, Dk. Mpango amehimiza pia umuhimu wa walimu kuwafundisha wanafunzi matumizi sahihi ya barabara.

“Serikali inatumia fedha nyingi kujenga barabara pamoja na kuweka alama za barabarani, hivyo wajibu wenu ni kuzitunza na kuzilinda ili zisiharibike kwa haraka,“ amesisitiza Dk. Mpango.

Pia amewataka wataalam wote wanaosimamia ujenzi huo kuhakikisha wanasimamia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati.

Aidha, kuhusu usalama barabarani Dk. Mpango ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuzingatia alama za barabarani ili kuepusha ajali na kuwaonya wale wanaohujumu alama za barabarani kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara ya Kazilambwa-Chagu (Km 36) na Ugansa-Usinge (Km 7.41) ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuifungua nchi katika kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi na hivyo kuleta tija kwa wananchi.

” Makamu wa Rais tumejipanga kuhakikisha mkoa wa Tabora na Kigoma inaunganishwa kwa lami katika kipindi kifupi kijacho na hivyo kuweka historia mpya kwa wananchi wa mikoa hiyo”, amefafanua Mhandisi, Kasekenya.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amesema ujenzi wa barabara ya Kazilambwa-Chagu (Km 36) ni sehemu ya barabara ya Kaliua-Malagarasi-Ilunde Km 156 ambapo kukamilika kwake kutaunganisha mkoa wa Tabora na Kigoma kwa lami na wamejipanga kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

Makamu wa Rais amemaliza ziara yake ya siku 3 mkoani Tabora kwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ikiwemo barabara, kwanja cha ndege, maji, umeme na majengo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here