Esther Mnyika, Dar es salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema serikali imejipanga kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025 kama ilivyokuwa uchaguzi wa mwaka 1995 ambao uliwezesha vyama vingi kuwa na wawakilishi.
Hayo ameyasema leo Oktoba, 8 jijini Dar es Salaam na Waziri Lukuvi alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha kwenye vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu amevipongeza vyama vya siasa nchini kwa kuendelea kulinda umoja na amani ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere.
Amesema hakuna haja ya vyama vya siasa kuwa na hofu ya kushiriki chaguzi hizo kwani maelekezo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa watendaji wote kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni kwenye kusimamia uchaguzi.
Amesema umoja na amani utaendelea kuimarika ikiwa kila chama cha siasa kitafuata salsafa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kutaka maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya.ambapo wasaidizi wake wote akiwemo yeye wanapaswa kutekeleza bila kupepesa macho.
“Rais Samia ameelekeza tusimamie uchaguzi kwa kufuata Katiba, Sheria na Kanuni na ameongeza 4R, hivyo haiwezekani mtu yoyote akiuke maelekezo yake,”amesema.
Lukuvi alisema Rais Samia mwakani anamalizia awamu yake ya kwanza na atashindana na vyama vingine kugombea awamu ya pili na mwisho hivyo vyama vya upinzani vijiandae kushindana kwa hoja na sera.
Aidha, Lukuvi akijibu hoja za chama cha NCCR Mageuzi alisisitiza uchaguzi utafanyika kwa kufuata kanuni zote ambazo zimepitishwa na vyama vyote.
Amewataka viongozi wa vyama vya siasa wapuuze kauli za wana CCM na viongozi ambao wanatoa kauli za kukatisha tamaa wananchi kushiriki uchaguzi.
“Narudia msisisitizo wa Rais ni vyama vyote vishiriki uchaguzi na kila atakayechaguliwa na wananchi ndiye atangazwe, hao wanajaribu kuharibu wapuuzeni,” amesema
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kutembelewa na Waziri Lukuvi viongozi hao waliihakikishia Serikali kuwa watashiriki na utakuwa ni uchaguzi wa utulivu kwa lengo la kulinda amani ya nchi.
Naye Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP), John Cheyo amesema UDP imejipanga kushiriki chaguzi zijazo iwapo mazingira yatakuwa rafiki kwa kila chama, huku akisisitiza kuwa wana imani na uongozi wa Rais Samia.
“United Democratic Party (UDP) sera yetu kubwa ni upendo na tunajua kuwa siasa si uadui na tutahakikiaha salsafa za Rais Dk.Samia zinatuongoza vyema ,”amesema Cheyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini amesema tangu mwaka 1990 hakuna waziri ambaye ameamua kujitambulisha kwenye vyama kama alivyofanya Lukuvi na kwamba mfumo umekuwa ukiwa ni wa vikao vya vyama vyote.
“Uamuzi wa Waziri umeonesha ana dhamira ya kweli ya kujenga siasa na kwamba wanaona mwelekeo mpya kwenye eneo hilo,”amesema.
Selasini amesema wapo katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo kuitaka serikali kusimamia ushindani sawa ambao itasababisha chaguzi kubwa huru na haki.
Pia ameiomba serikali kugharamia mchakato wa demokrasia ili kuhakikisha vyama vyote vinakuwa katika ushindani wa kweli.
“Huwezi kusema tunashindana kwenye uchaguzi wakati chama kimoja kinatumia ndege, magari na pikipiki, huku vingine vinatumia miguu kutafuta kura naomba upeleke ombi letu la kupata ruzuku,”amesema.
Amesema 2019 wagombea wa vyama vya upinzani walienguliwa bila utaratibu, hali ambayo ilisababisha vyama vingi kukosa nafasi ya kushiriki.
Amesema NCCR Mageuzi ipo tayari kushiriki siasa za maridhiano huku wakidai haki zingine ambazo zinakiuka katika mchakato wa kufanya siasa.
Mwenyekiti wa chama Cha wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba alisema anaishukuru Serikali kwa kuleta salsafa ya R4 ambayo ndani yake kuna maridhiano.
“Naona R4 zimeshaanza kufanya kazi yake hadi leo hii Waziri anatembelea vyama vya siasa ofisini kwao hayo ni mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya siasa,”amesema Profesa Lipumba.
Waziri Lukuvi ameanza Oktoba, 7 2024 ziara yake ya kutembelewa vyama vya siasa 19 ambapo leo ametembelea vyama vinne ambavyo ni chCUF, UDP,NCCR-Mageuzi na NLD.