Tabora
MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango amezipongeza Wizara za Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora.
Akizungumza leo Oktoba,9 2024 wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho Dk. Mpango amewataka wataalam wote wanaosimamia ujenzi huo kuhakikisha wanasimamia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati.
” Fedha hizi ni za wananchi hivyo zitumike vizuri kwa maendeleo ya wananchi”, amesisitiza Dkt. Mpango.
Aidha kuhusu usalama barabarani Dk. Mpango ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuzingatia alama za barabarani ili kuepusha ajali na kuwaonya wale wanaohujumu alama za barabarani kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 72 na ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.
“Makamu wa Rais ujenzi huu pia unahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, mnara wa kuongozea ndege, barabara za maingilio na maegesho ya ndege na barabara ya kuingia katika kiwanja cha ndege, maegesho ya magari, uzio wa usalama na Kituo cha hali ya hewa”, amefafanua Mhandisi Kasekenya.
Kiwanja cha ndege cha Tabora kilianzishwa mwaka 1940 na kimekuwa kikiboreshwa mara kwa mara na kukamilika kwake kutawezesha ndege nyingi kubwa kukitumia kiwanja hicho na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Tabora na ukanda wa magharibi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali itaendelea kuunganisha barabara za lami katika mikoa ya magharibi ili ifikike kwa urahisi na kuchochea shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kukuza uchumi wa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Mohamed Besta amesema ujenzi wa kiwanja hicho unatekelezwa na mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co, kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 24.6 .