Home KITAIFA WAZIRI LUKUVI AVITOA HOFU VYAMA VYA SIASA,NA WANANCHI KUHUSU CHAGUZI,

WAZIRI LUKUVI AVITOA HOFU VYAMA VYA SIASA,NA WANANCHI KUHUSU CHAGUZI,

Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amevihakikisha na kuvitoa hofu vyama vyote vya siasa nchini kuwa dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassani ,kuwa chaguzi zote zitakazofanyika chini ya Utawala wake zitakuwa huru na haki.

Hayo ameyasema leo Oktoba, 7 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea ofisi za vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kwa ikiwa lengo la kujitambulisha.

Pia aliviambia vyama hivyo kuwa vitisho vya watu sio vya Serikali wala mamlaka ila serikali inataka siasa zenye tija ambazo zitawaletea manufaa wananchi.

“Nawaondoa hofu wananchi kinachotakiwa siku ya kupiga kura nendeni mkapige kura na wakati wa kampeni hakikisheni mnasikiliza kwa makini sera na hoja kwa chama husika,”amesema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema kwa kutumia 4R za Rais Dk.Samia ikiwemo Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding) atahakikisha uchaguzi wa Serikali za mtaa unakuwa huru na wa haki.

“Ingependeza zaidi vyama vyote vya siasa vishindane kwa sera na hoja ili wananchi wapate nafasi nzuri ya kuwachambua na kujua ni nani wa kumpigia kura msidanganyike wananchi chaguzi zote zijazo zitakuwa huru na haki chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”amesema.

Akizungumza katika ziara hiyo Jaji Francis Mutungi amesema Waziri Lukuvi amekuja na utaratibu mpya na mzuri ambao unaonesha kuviweka pamoja vyama vya siasa.

Jaji Mutungi amevishukuru vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu ambavyo vimeonesha nia ya kukutana na Waziri.

“Utaratibu ulioanzishwa na Waziri Lukuvi ni mzuri na unaonesha utawajenga wanasiasa kuwa wamoja kwa lengo la kujenga nchi yetu na ziara iliyofanywa na Waziri Lukuvi inamanufaa mbalimbali ikiwemo kujua zilipo ofisi za vyama hivyo.,”amesema Jaji Mutungi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Pili Bara Chama cha ACT wazalendo Dorothy Semu alimshukuru Waziri Lukuvi kutembelea ofisi zao alisema ziara yake hiyo inajenga umoja ndani ya vyama vya siasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi cha Umma(CHAUMA), Hashim Rungwe alisema ni mara yake ya kwanza kuona waziri anatembelea ofisi za vyama tofauti amefurahishwa na jambo hilo.

Katika ziara hiyo vyama vilivyotembelewa jana ni Act-Wazalendo,CHAUMA,UPDP, na CCK. Ziara hiyo inaendelea leo na vyama vitakavyotembelewa ni UDP,NCCR –MAGEUZI,CUF na NLD.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here