Dar es Salaam
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema dhamira na malengo yake ni kujenga mfumo wa kodi utaokatenda haki ambapo kila anayestahili kulipa kodi alipe kwa stahiki yake na kiwango cha ulipaji kodi kwa Watanzania ni kidogo ambapo kati ya watu milioni 65 waliopo nchini wanaolipa kodi ni milioni mbili tu.
Dk. Samia ametoa kauli hiyo leo Oktoba, 4 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizindua Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo amesema ulipaji wa kodi ni msingi wa maendeleo.
“Tunataka kujenga mfumo wa kodi unaotenda haki, ambapo kila anayestahili kulipa kodi alipe kodi kwa stahiki na kodi zote zitozwe kwa mujibu wa sheria.
“Pia tunataka mfumo wa kodi unaochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na utakaochangia ujenzi wa uchumi jumuishi na unaowezesha serikali kutimiza malengo yake ya kuleta ustawi kwa wananchi,” amesema.
Amesema kodi ndio damu ya serikali hivyo hakuna mtu anayefanya kazi au biashara anayepata mapato halafu akaachiwa asilipe kodi.
“Kodi ndio damu ya serikali, kiukweli kabisa hakuna mtu anayefanya kazi, mtu anayefanya biashara, mtu anayepata mapato halafu aachiwe asilipe kodi ya nchi.Idadi yetu ya watu wanaolipa kodi ni watu kama milioni mbili kati ya watu milioni 65, idadi hii ni ndogo sana,” amesema Rais Dk. Samia.
Amesema uchumi unakua lakini hauakisi kinachokusanywa , kinakusanywa kidogo sana na kingi kinaingia katika mifumo ya watu bure tu.
Amesema pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanywa na mafanikio kupatikana lakini eneo la ukusanyaji kodi ni kubwa zaidi na muhimu ambalo anaamini litaleta mchango mkubwa zaidi ukuzingatia kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Shughuli za uchumi zinazoendelea nchini na idadi ya watu haiakisi mapato yanayopatikana, kwa mfano wigo wa vyanzo vya ndani vya kodi na visivyo vya kodi upo chini ya lengo tulilojiwekea,” amesema.
Rais Dk.Samia amesema miongoni mwa viashiria vya utulivu wa uchumi jumla vilivyoainishwa katika mpango wa tatu wa taifa wa miaka mitano ni pamoja na mwaka 2021/2022 na 2025/2026 ni pamoja na kuongeza mapato ya kodi hadi kufikia asilimia14.4 ya pato la taifa.
Amesema ifikapo mwaka 2026 kiwango hicho kitawapelekea kujitegemea zaidi katika ufadhili wa miradi ya maendeleo.
Rais Dk. Samia amsema kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) mwaka 2023/2024 mapato ya kodi yamefika asilimia12 ya pato la taifa hivyo bado kuna kazi ya kufanya.
Ameongeza kuwa kufuatia mashauriano na wadau mbalimbali serikali imeendelea kulifanyia kazi suala la kodi nchini pamoja na mambo mengine waliyofanya ni kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuijengea uwezo TRA.
Pia kuimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini ikiiwemo kufuta baadhi ya tozo na kuimarisha utendaji katika idara za serikali, wakala wa serikali na taasisi mbalimbali za serikali.
Amesema jitihada hizo zimeendelea kuleta matokeo chanya na kusababisha makusanyo ya kikodi kuongezeka kutoka wastani wa sh. milioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa sh. bilioni mbili kwa mwezi kwa mwaka 2022/2023.
Pia takwimu za makusanyo ya mwezi uliopita wa Septemba yalikuwa shilingi trilioni tatu na mabilioni kadhaa hivyo wanasonga mbele lakini kukiwa na kazi ya kufanya.
JAMBO LA KODI HALIJAWAHI KUWA RAHISI
Rais Dk. Samia alisema jambo linalichangia kwa namna moja au nyingine kufanya nchi itoke katika hatua moja hadi nyingine ni mifumo mizuri ya kodi.
Amesema kodi ilipwe kwa urahisi kwa kiwango cha juu yaani mfanyabiashara alipe mwenyewe kwa kiwango cha juu bila misukumano ili nchi ikusanye na iweze kuendelea.
“Sasa mkusanyiko wetu hapa(Ikulu) kuliangazia suala la kodi , kama mnavyojua jambo ambalo ni gumu sana kueleweka duniani ni hili la kodi, kodi ni suala gumu na hakuna anayelipenda, hasa kodi inayotokana na mapato yako.
“Mnawasikia wafanyakazi kila siku wanaaimba tupunguziwe kodi kubwa, lakini wafanyabiashara na wenyewe wanalalamika, wengine malalamiko kwa hiyo jambo la kodi halijawahi kuwa rahisi,” amesema.
UCHUMI JUMUISHI
Rais Dk. Samia amesema serikali inalenga kujenga uchumi jumuishi unaokuwa kwa kasi na unaoimarisha ustawi wa watu kwa kuboresha huduma za jamii na kupunguza umaskini wa kipato kwa mtu mmoja.
“Huku ndiko tunakoelekea sasa mambo yanayotakiwa kufanywa kufikia hatua hii kwanza ni amani na utulivu nchini, sisi Tanzania alhamdulilah tunao na tunajaribu sana kuhakikisha nchi inabaki na amani na utulivu,” amesema.
Amesema lipo suala la kuwa na mifumo ya haki inayoeleweka, katika kufanikisha ujenzi wa uchumi jumuishi unaokua kwa kasi na unaoimarisha ustawi wa watu.
“Katika suala la mifumo ya haki inayoeleweka tuliunda Tume ya kuangalia Haki Jinai ambayo na yenyewe ilifanya ‘study’ nchi nzima, kwenye vyombo vyote vya Haki Jinai na wametoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa mahakama wametekeleza vizuri sana kwani wako kwenye asilimia 70 ya utekelezaji , lakini vyombo vingine navyo kama jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya DPP na wengine nao wanaendelea kutekeleza,” amesema
SEKTA ZISIZO RASMI KUINGIZWA KATIKA MFUMO WA UCHUMI
Rais Dk. Samia amesema serikali itaiingiza rasmi sekta isiyo rasmi katika mfumo wa uchumi kutokana na kugundua kuwa katika pato la taifa malengo yaliyowekwa kutokufikiwa.
Amesema kilichosababisha hali hiyo ni mapato yote yanayokusanywa na sekta zisizo rasmi kumbukumbu zake kutoingizwa katika mpango wa Dira ya Maendeleo uliokwishafanyiwa tathmini unaotegemewa kumalizika mwaka 2025.
Pia amesema serikali ingekuwa na taarifa kamili ya sekta hizo zisizo rasmi basi kama sio kufikia lengo lingekaribiwa, kwani ufanisi umeshuka kwa sababu ya kutokuwa na data kamili ya sekta hiyo.
Amesema kutokana na hayo serikali inakwenda kuangalia namna ya kuingiza sekta isiyorasmi katika mfumo wa kiuchumi.