Dar es Salaam
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa ufafanuzi juu changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ya kuwepo kwa msongamano wa magari kwenye vituo vya kujazia gesi vilivyosababishwa na hitilafu ya umeme kwenye kituo cha Uwanja wa ndege .
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert.
Ufafanuzi huo umetolewa leo Oktoba 3,2024 jijini Dar es na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert amesema changamoto ya upatikanaji wa gesi asilia kwenye magari pia imechangiwa na ongezeko la matumizi ya gesi asilia kwenye magari hivyo kusababisha ongezeko la uhitaji wa nishati hiyo ukilinganisha na uchache wa vituo vya kujaza gesi.
“Baada ya changamoto ya tatizo la umeme katika Kituo cha Airport lililotokea usiku na kufanikiwa kurekebisha usiku wa siku iliyofuata vilibaki vituo viwili tu vya kujaza gesi, Kituo cha Tazara na Ubungo hivyo kusababisha uwepo wa foleni kubwa Kwa wateja wa wenye uhitaji wa kujaza gesi kwenye Vyombo vyao vya usafiri,“ amesema Mhandisi Emmanuel.
Aidha amesema wametoa fursa kwa makampuni zaidi ya 40 kuwekeza kwenye sekta hiyo lakini mwitikio bado umekuwa ni mdogo.
Ameeleza kuwa mpaka sasa kuna magari takribani 4,800 yanayotumia mfumo wa gesi asilia wakati uwezo wa vituo vitatu vilivyopo ni kujaza magari 1,200 mpaka 1,500 kwa siku, hali ambayo imekuwa ikisababisha foleni kubwa.
“Mikakati ya TPDC katika kutatua changamoto ya vituo ni kuendelea kujenga vituo vingine ambapo, Kituo kinachojengwa na TPDC eneo la Chuo Kikuu Dar es salaam kitakamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kitakuwa na pampu nne za kujaza gesi hivyo kupunguza foleni ya ujazaji gesi,”amesema.
Aidha amesema Kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza CNG kwenye magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku kitajaza zaidi ya magari 2000 na kitakuwa na uwezo wa kushindilia na kujaza gesi (CNG) kwenye malori matatu kwa wakati mmoja sawa na malori 24 kwa siku yatakayosafirisha na kusambaza gesi kwenye maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa TPDC kwa kushirikiana na Sekta binafsi ipo katika mkakati wa kukamilisha ujenzi wa vituo 13 vya kujaza gesi asilia kwenye magari ifikapo Julai mwaka 2025.