Home KITAIFA RAIS DK.SAMIA AMEZITAKA TAASISI ZA ELIMU NCHINI AMBAZO ZINAHUDUMIA WATU ZAIDI...

RAIS DK.SAMIA AMEZITAKA TAASISI ZA ELIMU NCHINI AMBAZO ZINAHUDUMIA WATU ZAIDI YA 100 KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Ruvuma

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za elimu nchini ambazo zinahudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia kwa lengo la kusapoti ajenda hiyo.

Pia amefurahishwa na matumizi ya nishati safi ya kupikia katika shule ya sekondari ya wasichana ya Dk. Samia na kwamba huo ni mradi wake alioubeba kwa wanawake wa Afrika.

Kauli hiyo aneiitoa leo Septemba, 27 wakati akizindua shule hiyo, iliyopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, na kusema wanawake wa Afrika wanapata maradhi kwa sababu ya kupika kwa kutumia kuni.

“Wanakufa kwa maradhi ya kupumua,upofu wa macho kwa sababu kuni mbalimbali zinatoa hewa au gesi mbalimbaliu ambazo zinawapa maradhi, mama zetu, bibi zetu waliumia katika hilo,” amesema.

Amesema wakati umefika wabadilishe na kutumia nishati safi ya kupikia kwa sababu lengo la mradi ni ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Sasa ili meseji hii iende vizuri tunaanza na taasisi za elimu kubwa, zile zinazoweka watu zaidi ya 100 ndizo tunazoanza nazo, nahakika wasichana ninyi mkiona mnavyopikiwa pale kwa gesi, chakula kilivyokitamu kilichopikwa na gesi, mnakua nayo na mnakwenda nayo mnakotoka na kuwaambia matumizi sasa ni gesi,” amesema.

Vilevile amewataka wanafunzi hao kuitumia vizuri elimu kwa kufanya vizuri katika masomo na mitihani kwani hatamani kusikia wamefanya vibaya.

Akizungumzia kuhusu teknolojia Dk. Samia amewasihi kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa manufaa ya maendeleo ya taifa kwa sababu ulimwengu umebadilika kila kitu ni teknolojia.

Ameeleza kuwa dunia kwa sasa imehamia katika akili bandia au akili unde kama ninavyopenda kuiita. Hatutatumia tena kalamu na karatasi kwa kiasi kikubwa, mambo mengi yatakuwa yanafanyika kwenye mtandao.

“Maswali mengi ya kitaaluma yanapatikana mitandaoni, kutumia zana kama Google ChatGPT  mtapata  majawabu ya masomo yenu, mkijifunza vizuri mtaona siri ya majawabu yote yako mtandaoni, mnapaswa kutumia fursa hiyo ipasavyo,” amesema.

Rais Dk. Samia amewataka walimu wa shule hiyo kuwajibika ipasavyo katika kutunza na kulea wanafunzi  waliowekwa chini ya uangalizi wao.

Amesisitiza kuwa wanalimu wanapaswa kuwa mstari wa mbele  kuhakikisha  wanafunzi wanajifunza vizuri na  wanatunzwa kiakili, kiafya na kijamii.

“Walimu tumewakabidhi watoto  wetu. Mazingira ya shule  ni mazuri, shule yenyewe ni nzuri na ingazwa tutahitaji kuongezeka, bado ninaomba sana  kuwa walimu muwatunze  watoto hawa.

“Mungu amewachagua  kuwa walezi wa hawa watoto  hakikisheni mnawajenga kielimu, kiafya na kuwawezesha kujitambua kama wanawake wenye uwezo wa kufikia ndoto zao,” amesema.

 Rais Dk. Samia amewakumbusha  walimu hao juu ya umuhimu wa kuwafundisha  wanafunzi  kutambua majukumu yao kama wanawake huku  akisisitiza  kuwa mwanamke anao uwezo  wa kufanya mambo yoyote  kama mwanaume.

Pia ametoa onyo kali kwa walimu  dhidi ya matukio ya wanafunzi kupata ujauzito na kusema watabeba lawama  endapo hilo litatokea.

“Hakikisheni mnalinda  maadili ya watoto wetu. Sitaku kusikia kesi ya mimba shuleni hapa, huku msitumi mimba itatokea wapi? ukitokea ujauzito walimu tutakabana  shingo kwa sababu huku msituni hakuna pa kutokea mimba,” amesema.

Rais Dk. Samia  amewahakikishia  walimu kuwa serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo ikiwemo uhaba wa maslahi na kuwataka kuwa na subra kwani serikali inaendelea kuzifanyia kazi.

Akizungumzia sekta ya elimu, Rais Dk. Samia  amesema jumla ya shule za msingi 16 na sekondari 14 zilijengwa, mwaka jana, mkoani Ruvuma.

Amesema hadi sasa mkoa wa Ruvuma unazo jumla ya shule msingi 860, kati ya hizo za serikali ni 815, shule 247 ni seko ndari huku 187 zikiwa za serikali.

Serikali imeendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo na sh. bilioni 14. 5 zimetolewa kwa mkoa huo huku akiupongea mkoa  kwa kuandikisha watoto 49,396 elimu ya awali, sawa na ongezeko la watoto 7,256 ikilinganishwa na mwaka jana.

Darasa la kwanza lilisajili watoto 52,636 na idadi ya watoto wa kike na kiume ikiwa sawa huku akiwataka wazazi kutorudi nyuma kuwapeleka watoto shule.

Amesema serikali itaendelea kutatua changamoto zitakazojitokekeza kadri mahitaji yanapoongezeka.

Rais Dk. Samia amewapatia  gari la shule baada ya kupokea changamoto kutoka wanafunzi hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alisema fedha zote za mradi wa majengo katika shule zilizopo nchini kwa asilimia 100 zilizokabidhiwa TAMISEMI zimetolewa kwa halmashauri zote.

Amesema shule hiyo pamoja na kuchukua watoto kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tano pia inachukua wenye uhitaji maalumu.

“Kwa kuwa kuna eneo kubwa katika shule hii wameanza kilimo cha mbogamboga ambacho watoto wameanza kulima ni maelekezo yako kwangu kuwa kwa shule zote 26 ubunifu huu uendelee kwa shule hizo nchini,” amesema.

Amemshukuru  Rais Dk. Samia kwa ubunifu huo kwani unakwenda kukwamua watoto wa kike nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here