Home KITAIFA MAJI, UZIO BADO TATIZO JOKATE MWEGELO SEKONDARI

MAJI, UZIO BADO TATIZO JOKATE MWEGELO SEKONDARI

Pwani

KUKOSEKANA kwa chanzo cha uhakika cha Maji kimetajwa kuwa kero sugu inayoikabili shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jokate Mwegelo (Kisarawe) kufuatia ongezeko la wanafunzi kila mwaka kutoka wanafunzi 80 shule ilipofunguliwa mwaka 2021 hadi kufika zaidi ya wanafunzi 800 mwaka 2024.

Uongozi wa Shule hiyo chini ya Mkuu wa Shule Mwalimu Mariam Mpunga, umesema kwamba licha ya jitihada zinazofanywa kuhikisha shule hiyo inaongeza ufaulu miongoni mwa watoto wa kike na kutokomeza Zero, Shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto za kimiundombinu na Mazingira ikiwemo, Kuwa na chanzo uhakika cha maji linakidhi ongezeko la wanafunzi.

Changamoto zingine ni Ukosefu wa uzio wa shule kwa ajili ya ulinzi na usalama wa watoto wa kike ikizingatiwa kuwa shule hiyo ipo kijijini pembezoni kabisa mwa mji wa kisarawe ambapo imezungukwa na pori hali inayopelekea wanafunzi kuwa na hofu ya kuvamiwa na wadudu na wanyama hususani nyakati za usiku.

Pia Mwalimu Mpunga amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na ukosevu wa makazi bora ya walimu, Maabara kukidhi ongezeko la idadi ya wanafunzi, Gari la shule panapotea hali ya ugonjwa wa dhararu ikizingatiwa kuwa shule hiyo iko pembezoni kabisa na Mji wa Kisarawe katika Kata ya Kibuta.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kisarawe, (Khalfani Sika) kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (Jokate Mwegelo) amesema tayari Serikali imetoa shilingi Milioni 90 kwa ajili ya ukamilishaji wa Bwalo, na shilingi Milioni 30 kwa ajili ya upanuzi wa Maabara

Ametoa rai kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuona unyeti changamoto hizo na kutenga bajeti Maalum kujenga uzio shuleni hapo ili kuwapa watoto wakike hali ya kujiamini katika mazingira ya kujifunza na kujifunzia.

Awali akizungumza na wazazi katika hafla ya kuwaaga Kidato cha Nne, Afisa Elimu Idara ya Sekondari Mwalimu Editha Fue, amewasihi wazazi kuwajibika ipasavyo kuwalinda wanafunzi wawapo majumbani dhidi ya ukatili na Vishawishi hatarishi na kuhakikisha wanayaishi na kuyaendeleza yale yote waliyojifunza shuleni.

Shule ya Sekondari wasichana Jokate Mwegelo (Bweni) ilianzishwa Mwaka 2021 kufutia Vuguvugu la ‘TOKOMEZA ZERO KISARAWE’ lililoasisiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa wakati huo, Jokate Mwegelo, ikilenga kuondoa kabisa daraja SIFURI katika Matokeo ya Elimu ya Sekondari na kuongeza ufaulu kwa mtoto wa Kike ambapo hadi sasa Shule hiyo imeshatoa wahitimu wa kidato cha sita kwa awamu mbili (2023 na 2024) bila kuwa na mwanafunzi yeyote aliyepata daraja SIFURI na ikitarajia kupata wahitimu wa kidato cha NNE kwa mara ya Kwanza Mwaka huu (2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here