Ruvuma
RAISI Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inatarajia kufungua vituo 100 vya kufundisha lugha ya kiswahili duniani huku amewataka Watanzania kutumia fursa kujiingizia kipato.
Pia Rais Dk.Samia amewasihi watanzania kuwakataa wale wote wanaowataka kuwagawa watanzania kwa maslahi binafsi huku kutanguliza maslahi mapana ya nchi.
Hayo ameyasema leo Septemba, 23 2024 Dk.Samia wakati wa kilele cha Tamasha la Tatu la Utamaduni Kitaifa lilofanyika katika uwanja wa Majimaji Songea Mkoani Ruvuma.
“Ndugu zangu wana Ruvuma na Watanzania, utamaduni una masuala mengi maana unahusu namna tunavyoishi, kwetu sisi hatuwezi kuongelea utamaduni wetu bila kugusia lugha yetu pendwa ya Kiswahili ndio lugha inayotuunganisha na kuwa na utamaduni mmoja na lugha hii imefungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania. Kwa kuzingatia hili, Wizara imenijulisha kwamba mwaka huu wamenijulisha kufungua vituo 100 vya lugha ya Kiswahili kote duniani kwa kushirikiana na Diaspora yetu,” amesema Rais Dk. Samia.
Vilevile amewatake watanzania kutanguliza maslahi ya nchi kabla ya maslahi binafsi tuwakatae wote wanaotaka kutugawa kwa sababu za kisasa au tofauti za kiitikadi watanzania ni wamoja na Tanzania ni moja.
Amesema kutokana na mwingiliano wa teknolojia kumeanza kushuhudiwa momonyoko wa maadili miongoni mwa watanzania na vitendo visivyofanana na utamaduni wetu.
Amefafanua kuwa jambo hilo linaanzia ngazi ya familia ametoa rai kwa kila mtanzania kubeba jukumu la maadili katika boma lake amefurahi kuona viongozi wa kimila mahali hapo kwa sababu anaamini kwa kushirikiana na viongozi wa dini watafanikiwa kushughulikia suala la momonyoko wa maadili.
Rais Dk. Samia amewakumbushe watanzania kuwa mwezi Novemba mwaka huu tutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za mitaa. Kipindi cha uchaguzi ni fursa wanayowapa wananchi kupiga kura ya kupata viongozi watakaowakilisha katika nafasi mbalimbali za uongozi ili watusaidie kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa letu.
Aidha ameongeza kuwa michezo ni sehemu ya utamaduni wetu ni fahari kuwambusha kuwa nchi yetu imepata dhamana kama alivyosema Waziri hapa dhamana kubwa kwa kushirikiana na wenzetu wa Kenya na Uganda kuandaa mashindano ya AFCON mwaka 2027.
“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi kuelekea mashindano hayo pamoja na viwanja vingine vilivyopo pia tunafanya ujenzi wa viwanja ambavyo ujenzi unaendelea na hapa hivyo ujenzi wa kiwanja kule Arusha unaendelea vizuri. Nitoe rai kwa Watanzania kuwa AFCON ni fursa kubwa kwetu kuanzia wajasiriamali wa kazi za ubunifu, utamaduni, sanaa na michezo na Watanzania wote,” ameeleza.