Home KITAIFA WAZIRI GWAJIMA AZINDUA MRADI WA BILIONI 8 WA USAID WANAWAKE SASA KULETA...

WAZIRI GWAJIMA AZINDUA MRADI WA BILIONI 8 WA USAID WANAWAKE SASA KULETA CHACHU USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI.

📌Unaunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya kuleta usawa wa kijinsia katika Dira ya Maendeleo ya Taifa.

📌Unaenda sambamba na Falsafa ya 4Rs za Rais Samia

Dar es Salaam

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima amesema Mradi wa Wanawake unaotekelezwa Shirika la WiLDAF kwa kushirikiana na Mashirika ya Her Initiative na Jamii Forums, kwa ufadhili wa Watu wa Marekani (USAID) wenye thamani ya shilingi Bilioni 8.1 utaleta chachu na kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika masuala ya uraia, siasa na uchaguzi.

Dk. Gwajima ameyasema hayo jijini Dar es Salaam Septemba 19, 2024 wakati akizundua Mradi wa Wanawake Sasa wenye Kaulimbiu isemayo; Wanawake na Wasichana Wana Haki ya Kushiriki katika uongozi na Michakato ya Demokrasia.

Amesema malengo ya mradi huo yanaunga mkono juhudi za Serikali ya kuleta usawa wa kijinsia kwenye nyanja zote kama ilivyobainishwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Pia malengo haya yanaenda sambamba na Falsafa ya 4Rs (Reconciliation (Maridhiano), Reforms (Mabadiliko), Resilience (Ustahimilivu) na Rebuilding (Kujenga Upya) ambayo yanaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ameeleza mradi huo utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uwezo na ari ya wanawake kushiriki kwenye masuala ya uraia na siasa na kugombea nafasi za uongozi, kuwashirikisha wanaume kama vinara wa kushawashi usawa wa kijinsia, kuongeza uelewa na uwezo wa masuala ya usawa wa kijinsia kwa watendaji kutoka vyama vya siasa, taasisi za Serikali na vyombo vya usimamizi wa uchaguzi na masuala ya siasa nchini.

Ameongeza kuwa pia mradi huo utasaidia kuboresha uwezo wa Asasi za Kiraia za Vijana, Wanawake na Watu Wenye Ulemavu kuchagiza ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya uraia, siasa na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Sote tunatambua utashi na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza usawa wa kijinsia kupitia sera, sheria na mipango mbalimbali. Pia Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya wanawake ya mwaka 2023 katika sura ya 3.2.4 imeweka tamko la kukuza uelewa kwa jamii kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika ngazi zote za uongozi na maamuzi na kukuza usawa na ushiriki jumuishi wa wanawake ,wanaume ,wasichana na wavulana,” amesisitiza Dk. Gwajima.

Vilevile amesema Wanawake wanaweza mfano mzuri ni Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa awamu ya sita kwa uhodari wake wa kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati kuhamasisha masuala mbalimbali katika jamii ikiwemo michezo ambapo, soka (mpira wa miguu), tumeshinda kuandaa mashindano ya Afrika (AFCON) kwa mwaka 2027.

“Kule Bungeni tunaye, Dk. Tulia Ackson anayepeperusha bendera akiwa Raisi wa Mabunge Duniani tunaona utendaji wao, vijana wa siku hizi wanasema wanaupiga mwingi. Sioni hoja ya kwanini vyama havitapendekeza wagombea wanawake kwenye chaguzi zijazo,” ameeleza Dk. Gwajima

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Wanawake Sasa Anna Kulaya amesema watahakikisha mradi huo unaleta matokeo chanya kwa kutoa elimu kwa jamii hasa watoto wa kike na Wanawake katika kujua kuwa ni haki yao kushiriki katika kugombea katika nafasi za uongozi siasa na nafasi za maamuzi.

“Leo hii tunayofuraha kusema mradi huu utaleta chachu katika mabadiliko ya fikra na tunaomba tuendelee kupata ushirikiano kutoka katika Taasisi za Kiserikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine,” amesisitiza Anna.

Ameongeza kuwa katika harakati za Wasichana na Wanawake Tanzania imekua Nchi ya kwanza Afrika kutambua unyanyasaji wa kijinsia kuwa kosa katika masuala ya Uchaguzi hivyo itasaidia kuleta chachu na kuwainua Wanawake na Wasichana katika kushiriki kugombea nafasi za uongozi na maamuzi.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania Craig Hart amesema Mradi huo ukitekelezwa kama ilivyopangwa utaleta mabadiliko hasa kwa jamii katika kubadili mitazamo na kuwapa nafasi Wasichana na Wanawake kushiriki katika siasa na kugombea nafasi za uongozi na maamuzi katika maeneo yao.

Pia Mrajisi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Zanzibar Ahmed Khalid Abdula amesema wameipokea Mradi huo kwa upande wa Zanzibar na watahakikisha mradi huo utafanikiwa kwamkitoa ushauri na maelekezo ili mradi lengo lake litimie na Wanawake na Wasichana katika kushiriki katika siasa na kugombea nafasi za uongozi na maamuzi hasa kwa kupata nafasi katika Vyama vya Siasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here