📌Kapinga asema lengo ni kuwafanya Watanzania zaidi ya asilimia 80 kutumia nishati safi ifikapo 2034.
📌Kwa mwaka huu wa fedha mitungi laki nne kutolewa.
📌Atoa rai kwa Watanzania kuendelea kuhamasishana matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Geita
NAIBU Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia utakaowafanya watanzania zaidi ya asilimia 80 kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
Kapinga ameyasema hayo leo Septemba 19, 2024 katika Kongamano la wanawake na mabinti mkoani Geita lenye lililokuwa na lengo la kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia, kujadili mada mbalimbali ikiwemo mwanamke na maendeleo.
“Tunahamasisha matumizi ya nishati safi ya ili kulinda afya za watanzania, kuboresha uchumi na kutunza mazingira ambayo yamekuwa yakiharibiwa kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia,” amesisitiza Kapinga.
Ameongeza kuwa ili kurahisisha matumizi ya nishati safi ya kupikia Serikali imetoa ruzuku kwenye mitungi ya gesi ambapo kwa mwaka jana ilitoa mitungi laki moja na elfu nne na mwaka huu wa fedha Serikali inategemea kutoa mitungi laki nne.
Aidha, Serikali kuendelea kuhakikisha Taasisi zenye watu zaidi ya 100 zinaendelea kubadilishana mfumo na kutumia gesi.
Kapinga ameongeza kuwa nishati safi za kupikia zipo za aina nyingi ikiwemo gesi, majiko banifu, umeme, majiko ya ethanol na majiko mengine yaliyoboreshwa na kuwa ya nishati safi.
Ametoa rai kwa Watanzania kubadilisha fikra kuwa mapishi ya nishati safi ni gharama na kusisitiza kuwa majiko ya siku hizi yameboreshwa hayatumii umeme mwingi.
Aidha, Serikali inaendelea majadiliano na wadau ili wananchi waweze kununua gesi kidogo kidogo ili kumwezesha mtanzania kununua gesi kulingana na kiasi cha fedha alichonacho.
“Kila mmoja analojukumu la kulinda mazingira kwa ajili ya mama Tanzania, nitoe rahi tuendelee kuhamasishana juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia,”amesema Kapinga.