Home KITAIFA SERIKALI YA SMT NA SMZ ZITAENDELEA NA JUHUDI ZA KUIMARISHA DHANA YA...

SERIKALI YA SMT NA SMZ ZITAENDELEA NA JUHUDI ZA KUIMARISHA DHANA YA UFUATILIAJI NA TATHMINI KWA PANDE ZOTE MBILI ZA MUUNGANO

Zanzibar

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zitaendelea na juhudi za kuimarisha dhana ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa pande zote mbili za Muungano hasa katika shughuli za Mipango ya Kitaifa na Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba, Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Kongamano la Tatu (3) la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi liliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar Septemba, 17 2024.

Amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua katika uimarishaji wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini ikiwemo kuweka mifumo na miundombinu yenye kuwezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa Taasisi za Kitaifa zinazoratibu masuala hayo kwa maslahi mapana ya nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed amesema matumizi ya Teknoloji katika kufanya ufuatiliaji na Tathmini kutaiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuimarisha uwajibikaji na kuongeza kasi na uwazi katika kuleta ustawi wa wananchi kwa kutoa huduma sahihi za kijamii na kiuchumi.

Amesema kuwa anatambua kuwa mafanikio makubwa yamepatika katika shuhuli za ufuatiliaji na tathmini nchini hivyo amezitaka Mamlaka husika kufanya jitihada za kukamilisha maandalizi ya Sera za Ufuatiliaji kwa Serikali zote mbili pamoja na kutenga rasilimali za kutosha kuwezesha utekelezaji wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini.

Aidha amezitaka Taasisi hizo kuhakikisha taarifa zinazozalishwa kutokana na kazi za ufuatiliaji na tathmini zinatumika katika kufanya maamuzi na kuweka mikakati imara ya kuhabarisha Umma juu ya matokeo ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa kushirikiana na waandishi wa habari ili kufikia malengo ya taasisi na Taifa kwa ujumla .

Hemed ametoa wito kwa chama cha Wataalamu Afrika(AFrEA) kuendelea kuvilea vyama vidogo vidogo vilivyomo nchi wanachama pamoja na kuapta fursa za kujifunza na kujiimarisha ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,William Lukuvi amesema katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kunahitaji uwepo wa taasisi zenye kufanya Ufuatiliaji na Tathmini ili kusaidia kulinda matumizi ya rasilimali fedha zinazotumika katika miradi hiyo.

Lukuvi amesema kuwepo kwa Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza vinaakithi dhamira ya Serikali zote mbili ya kuhakikisha mabadiliko na marekebisho makubwa yanafanyika katika kuimarisha Teknolojia na mifumo ambayo itasaidia kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali hizo kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji (SMZ), Sharif Ali Sharif amesema kufanyika kwa Kongamano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza hapa Zanzibar litaibua na kupendekeza njia nzuri zaidi za kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini hasa katika masuala ya Utalii na Uwekezaji nchini.

Amesema kufanyika kwa Ufuatiliaji na Tathmini kunasaidia katika kupima shuhuli za mipango ya maendeleo ya Kimataifa, kitaifa na Kikanda kwa kutathmini ufanisi na uwajibikaji wa Taasisi husika hasa katika kupata taarifa na Takwimu sahihi zenye matokeo chanya ya mipango hiyo.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi akieleza kuhusu kongamano hilo amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu makongamano hayo ikiwa hilo ni la Tatu kufanyika na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 650 na kusema ni ongezeko kubwa linaloonesha muamko kwa washiriki kwa kulinganisha awamu zilizopita ambapo Awamu ya kwanza walijitokeza washiriki 302, awamu ya pili washiriki 624.

“Lengo ni kuendeleza jitihada za Serikali za kujenga uelewa na utamaduni wa ufuatiliaji na tathmini kwa watendaji wa Serikali, Wadau na Jamii kwa ujumla. Hivyo, Kongamano hili linawakutanisha wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, na wadau wa Serikali na sekta binafsi wakiwemo watunga sera, watekelezaji sera na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu,” amesema.

Ameongezea kuwa Kongamano hilo linatoa fursa ya kukumbushana juu ya umuhimu na faida za ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali.

“Ni matarajio yetu kongamano litaleta matokeo mengi ikiwemo kuongeza ubunifu katika utendaji wetu, matumizi ya TEHAMA pamoja na kuongeza weledi katika dhana hii ya ufuatiliaji na tathmin,”alisema Dk. Yonazi

Kwa upande wake Mwakilishi wa USAID Tanzania Craig Hart ameeleza kuwa uwepo wa kongamano hilo unatarajiwa kuleta matokezo zaidi katika shughuli za kila siku kwa kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya kisasa.

“Hakika wiki hii ni matarajio yetu ilete matokeo yanayotarajiwa hivyo litumike kwa usahihi hasa kujifunza na kuona namna ya kujitathim namna tunavyofanya kazi na ujuzi huu utumike kwa kuimarisha utendaji kazi, tunaahidi kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada wakati wa Kongamano hilo amesema kuwa,tathimin na ufuatiliaji ni jambo la msingi hivyo linapaswa kuendelea kupewa kipaumbele kwa lengo la kusaidia namna ya kuendelea kuzitumia malighafi tulizonazo, hivyo ni eneo muhimu sana katika shughuli zetu za kila siku.

“Ufuatiliaji na tathmini ndiyo njia pekee inayotusaidia kujua nini kiboreshwe na wapi penye kuhitaji mkazo kwa kuzingatia umuhimu wake, hivyo hii ndiyo engeene muhimu yenye kutupa uwezo wa kujitathmin,” amesema Profesa Elisante.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here