Pwani
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 830 kwa ajili ya kujenga upya na kwa ubora zaidi barabara na madaraja yalioathiriwa na mvua za El -Nino na kimbunga Hidaya nchini kote .
Hayo yamesemwa leo Septemba, 17 2024 na Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami inayojengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group (CRSG), na kuhimiza umuhimu wa ujenzi huo kuwiana na thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na mradi huo mapema iwezekanavyo.
“Pesa ambayo tumetafuta kwa ujumla wa Tanzania nzima haitakuwa chini ya shjilingi bilioni 830 kwahiyo unaweza ukaona sio hela ndogo
“Niwahakikishie Rais ameshatoa fedha hizi, kazi iko kwetu Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuhakikisha wakandarasi makini wanapatika kujenga miundombinu hii iliyoathiriwa na mvua”, amesema Mhandisi Kasekenya.
“Tupo katika hatua za mwisho ili wakandarasi waingie kazini kwani Mheshimiwa Rais ametupa muda maalumu tuhakikishe ndani ya muda huo kazi iwe imekamilika yaani kazi haitasimama,” amesema.
Amesema fedha hizo ni kwaajili ya kufanyia ukarabati madaraja yote nchini yaliyoathirika kwani kuna madaraja mengi yaliharibika lakini Dk. Samia ametoa fedha ya kuyajenga upya nchi nzima
“Tuna kwenda kujenga pale palipokuwa karavati la mita mbili tutaweka daraja la mita tano, daraja lenye upana wa mita 20 tutajenga mita 40 baada ya kujifunza kwamba hayamaji yanaweza kuja kwa kiasi kikubwa sana.
“Watanzania naomba walielewe hilo kwamba kote kulikokuwa kumekatika tunakwenda kujenga upya na kwa ubora zaidi ili turudishe miundombinu ya barabara zetu katika ubora wake,”amesema.
Aidha, Kasekenya amesisitiza umakini na kasi katika ujenzi wa daraja la Mbambe lenye urefu wa mita 81 linalounganisha mji wa Ikwiriri na Mkongo pamoja na barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami ili zikamilike haraka na kuchochea shughuli za usafiri na usafirishaji wilayani Rufiji.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewahakikishia wakazi wa Kilwa, mkoani Lindi kuwa barabara ya Tingi-Kipatimu itajengwa kwa lami kwa awamu huku madaraja katika barabara hiyo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwezi Oktoba, 2024.
“Fedha hizo kwakuwa changamoto iliyokuwepo ni ya dharura serikali ya Tanzania itashirikiana na Banki ya Dunia,”amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Brabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage amesema ujenzi wa barabara hiyo una jumla ya makalvati 109 ambapo kati ya hayo mawili yamekamilka na ujenzi wa kalvati moja unaendelea.
Mhandisi Kasekenya ameendelea na ziara yake katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara na madaraja hususan yalioathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.