Kilimanjaro
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha kuwa yeye ni kiongozi madhubuti anayeweka maslahi ya Tanzania mbele.
Akizungumza leo Septemba 17 2024 mkoani Kilimanjaro Rais Dk. Samia kwenye hafla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Maofisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, hafla ambayo pia iliadhimisha miaka 60 ya Jeshi hilo, amewapongeza askari wa polisi kwa kazi yao kubwa ya kulinda amani na utulivu wa taifa letu.
Rais amethibitisha kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Rais Dk.Samia ameweka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayojitegemea na yenye hadhi, na hivyo haiwezi kuamriwa na watu wa nje kuhusu jinsi ya kuendesha masuala yake ya ndani.
Pia amekemea vikali kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya balozi za kigeni baada ya kifo cha mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ali Kibao.
Amefafanua kuwa kauli hizo hazikutolewa kwa ridhaa ya serikali za balozi hizo, na akasisitiza kuwa balozi hizo zinapaswa kuheshimu mamlaka ya Tanzania kama vile balozi zetu zinavyoheshimu mamlaka za nchi nyingine.
“Hatutaruhusu kamwe mataifa ya nje kutuamulia.
“Alifichua njama zinazofanywa na chama kimoja cha upinzani ambacho kilifanya mkutano huko Arusha ta Septemba, 11 2024 ambapo ajenda kuu ilikuwa ni jinsi ya kutumia maandamano na vurugu ili kuvuruga serikali kwa matumaini ya kuipindua,” ameeleza Dk.Samia.
Amesema jambo hilo ni hatari na linaweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu, jambo ambalo Rais alilieleza kwa uwazi kabisa.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa macho na kuepuka kujiingiza kwenye njama hizi za kipumbavu zinazoweza kuleta machafuko.
Rais Dk.Samia ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kuheshimu falsafa yake ya 4R’s (Maridhiano, Uvumilivu, Haki na Uwajibikaji) na kutochukulia kimzaha uhuru wa kisiasa wanaoufurahia sasa.
Amewakumbusha kuwa, uhuru huo wa kisiasa umepatikana kwa jitihada kubwa, na hivyo ni muhimu kuutumia kwa busara, si kwa kuchochea vurugu na machafuko.
Kwa ujumla, hotuba ya Rais Samia imeendelea kudhihirisha uimara wa uongozi wake na dhamira yake ya kulinda taifa dhidi ya vitisho vyovyote vya ndani na nje.
Rais Dk. Samia amesema Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu chini ya uongozi wake, huku amehakikisha kuwa wale wanaotaka kuiyumbisha nchi wanadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.