Home KITAIFA WAZIRI MAVUNDE AYATAKA MAKAMPUNI YA MAKAA YA MAWE KUWEKEZA KATIKA UZALISHAJI WA...

WAZIRI MAVUNDE AYATAKA MAKAMPUNI YA MAKAA YA MAWE KUWEKEZA KATIKA UZALISHAJI WA UMEME

_Aipongeza Ruvuma kwa kuvuka lengo la Ukusanyaji Mapato kwa asilimia 112 miezi miwili ya kwanza Mwaka 2024/*

_Apongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye uzalishaji wa makaa ya mawe

Aagiza Makampuni kuzingatia Sheria za Uwajibikaji wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR)

Ataka wazawa kupewa kipaumbele kwenye Utoaji huduma migodini (local content)

Ruvuma

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amezipongeza Kampuni za uzalishaji wa makaa ya mawe kwa kuongeza uzalishaji na kuzitaka kuelekeza zaidi uwekezaji wao katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini.

Ameyasema hayo leo Septemba, 16 2024 Mkoani Ruvuma alipokuwa akizungumza katika Mkutano na Wadau wa Makaa ya mawe baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua migodi ya uzalishaji wa makaa ya mawe iliyopo Kata ya Luanda Wilayani Mbinga.

Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa biashara ya Makaa ya Mawe imechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa Sekta ya Madini hapa nchini, na kwamba Serikali inatambua mchango wa Wawekezaji wa makaa hayo katika maeneo tofauti nchini ikiwemo Wilayani Mbinga.

“Mafanikio haya yametokana na mazingira wezeshi ya uwekezaji chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo yamevutia na kusaidia kupatikana Wawekezaji Wakubwa katika Sekta ya Madini pamoja na nyingine za kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya matokeo ya Falsafa ya 4R iliyo nguzo muhimu katika kuvutia uwekezaji huo nchini,” amesisitiza Mavunde.

“Kwa mujibu wa Shirika la Takwimu Tanzania (NBS) na Wizara ya Madini, Sekta ya Madini nchini imekuwa kwa kasi kwa mwaka 2024, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kufikia lengo la kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP) ifikapo mwaka 2025. Pamoja na Marekebisho ya Sera na Sheria za Madini ili kuhamasisha uwajibikaji, Sababu nyingine zinazochangia ukuaji wa Sekta hii ni pamoja na ongezeko la mauzo ya madini nje ya nchi, hasa dhahabu na makaa ya mawe, ambayo yanachimbwa hapa kwa wingi, hongereni sana,” amesema Mavunde.

Ameongeza kuwa, Makaa ya Mawe yanayopatikana Mbinga yana ubora wa kiwango cha juu kuliko yanayopatikana katika maeneo mengine hapa nchini.

Aidha, amesema kuwa uwepo wa miradi hiyo imesaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira kwa wenyeji wa Wilaya ya Mbinga, hali ambayo imebadilisha maisha ya watu wa eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameupongeza Mkoa wa Kimadini wa Ruvuma kwa kuvuka lengo la Ukusanyaji Mapato ya Serikali kwa asilimia 112 katika miezi miwili ya kwanza kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na kuwataka kuongeza juhudi zaidi.

Amesisitiza kuwa ipo fursa kubwa ya kuzalisha umeme kutoka kwenye makaa ya mawe, na kwa kuwa dunia hivi sasa inaelekea kwenye matumizi ya nishati safi, makampuni badala ya kusafirisha makaa nje kuwekeza kwenye uzalishaji wa umeme, jambo ambalo litaiwezesha Tanzania kuendelea kutumia rasilimali zake kwa njia endelevu huku ikikidhi mahitaji ya nishati safi na kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kisare Makore ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa ikisumbua kutokana na wingi wa vumbi na kwamba Serikali ni sikivu na inajali wananchi wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini,Jonas Mbunda wameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kutatua changamoto ambazo zinalalamikiwa na Wananchi wanaozunguka miradi hiyo na Wawekezaji wanaendesha shughuli zao za uzalishaji katika Wilaya hiyo na kusaidia kuchagiza maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here