Home KITAIFA PROGRAMU YA AJIRA SAWA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA SEKTA BINAFSI – WAZIRI...

PROGRAMU YA AJIRA SAWA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA SEKTA BINAFSI – WAZIRI DK. GWAJIMA

Dar es Salaam

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amezindua Programu ya Ajira Sawa inayowalenga wanawake walio kwenye sekta binafsi katika kukuza usawa wa kijinsia.

Waziri Dk. Gwajima akizungumza na wadau walioshiriki uzinduzi huo jijini Dar es Salaam Septemba 12, 2024 amesema Programu hiyo inayotekelezwa na Benki ya Dunia kupitia Taasisi ya IFC iliyo chini yake inayoshughulikia masuala ya Jinsia pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), nisehemu ya matokeo ya jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuwakomboa wanawake na kuongeza mchango wao katika ujenzi wa Taifa.

“Tanzania kupitia mikataba, itifaki na Maazimio ya Kimataifa na Kikanda, inatekeleza Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa ambapo Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kinara wa utekelezaji wa Jukwaa hilo hususan kuhusu haki na usawa wa kiuchumi. Chini ya Jukwaa hili, imetengenezwa Programu ya ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi hivyo, kuzinduliwa kwa Programu hii kunaendana na malengo ya ahadi za nchi kwenye jukwaa hilo na kutachochea kuboreka hali ya wanawake walio kwenye sekta hii ifikapo mwaka 2026.” amesema Dk. Gwajima.

Aidha, amebainisha kuwa hadi sasa utekelezaji wa mpango wa tatu wa Taifa wa Ujumuishwaji wa Huduma ya Fedha kwa mwaka 2023-2028 pamoja na mambo mengine unaweka kipaumbele kwenye ujumuishwaji wa wanawake kwenye sekta rasmi ya kifedha na hadi sasa utekelezaji wake umewezesha kupunguza pengo la kijinsia kutoka asilimia 9 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3 mwaka 2023 (Finscope 2023).

Ameongeza kuwa, hali hiyo inamaanisha wanawake wengi wanazidi kupata fursa kwenye mfumo rasmi wa kifedha ikiwemo kupata mitaji.

Dk. Gwajima ameeleza pia, Serikali kupitia Sheria ya manunuzi kwa mashirika ya umma, imeweka wazi asilimia 30 ya mikataba yote ya manunuzi ya umma kila mwaka iende kwa wanawake na makundi maalum ambapo wanawake wachache wamejitokeza, hivyo anaamini programu hiyo utasaidia kujenga uwezo wa wanawake wengi kufikia fursa ya kutekeleza huduma na miradi kwa zabuni za Serikali.

Amesema Programu hiyo itaongeza kasi ya kuwafikia wanawake wengi zaidi kwa kuwa mchango wa nguvukazi ya wanawake bado unazoroteshwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutojumuishwa ipasavyo katika Sekta ya binafsi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Susanne Ndomba amesema Mipango mahususi iliyopo ni pamoja na kukuza fursa sawa za ajira, kuendeleza wanawake katika uongozi kupitia na kusaidia wanawake wajasiriamali sio tu wa kimkakati lakini pia itachangia kuondoa vikwazo ambavyo wanawake wanakumbana navyo katika sehemu za kazi na kuwawezesha kustawi.

Kwa upande wake Mkuu wa Program ya Jinsia wa IFC Anna Mushi amebainisha ni Asilimia 10 tu ya wanawake ndio wapo kwenye mfumo rasmi wa fedha nchini hivyo mradi huo wa miaka mitatu utafanya kazi na kampuni binafsi kuhakikisha usawa katika hilo na kuwahamasisha sekta hizo kujiunga na programu ili kusaidia wanawake kufikia fursa katika sekta binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here