Dar es Salaam
KAMISHNA Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Abdallah Mpallo amesema jamii ijitokeze kupima afya kwenye kambi zinazokuwa kimeandaliwa ili kuikomboa afya na magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.
Mpallo ambaye pia anatoka kikosi cha afya amesema katika kuelekea kilele cha wiki ya Polisi shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za Afya kwa kupima magojwa mbalimbali.
Mpallo ameyasema hayo leo Septemba 11, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akimuwakilisha Kamanda wa Kikosi cha Afya Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Lucas Mkondya.
“sisi kama kikosi cha polisi tumelenga kutoa huduma za vipimo bure kwa watu wote ili kutambua afya zao na endapo mtu atagundulika kuwa anahitaji matibabu makubwa zaidi atapewa rufaa ya kwenda hospitali kubwa ilikuendelea na matibabu zaidi. Pia tunatoa elimu kuhusu magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza hasa namna ya kijikinga na homa ya nyani (Mpox),”amesema.
ACP. Mpallo amesema katika kambi hiyo itatolewa elimu hukusu mguu kifundo kwani watu wengi uamini kuwa ulemavu huo unasababishwa na imani za kishirikina.
“Kikosi cha Afya kitatoa elimu juu ya mguu kifundo kwani watoto wengi huzaliwa wakiwa na ulemavu huo lakini wazazi wao hudhani kuwa hiyo ni laana bali ni mapenzi ya Mungu lakini pia kuna hospitali nyingi ambazo zinafanya upasuaji wa kuondoa mguu kifundo,”amesema.
Mpallo amesema huduma hizo zinatolewa katika hospitali ya mkoa wa kipolisi Kurasini na akatumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuachana na mila potofu kwani mila hizo zinarudisha maendeleo nyuma huku akiwakaribisha polisi na wananchi wote kushiriki katika maadhimisho hayo.
Maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa Polisi yenye kauli mbiu”Elimu ya afya, huduma bora ya kipolisi kwa umma itapatikana kwa kubadilika kifikra, usimamizi wa sheria na matumizi ya tehama”yalianza septemba 2 na yanatarajiwa kuhitimishwa septemba, 13 mwaka huu.