Na. Saidina Msangi, Mkuranga Pwani.
TIMU ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, imewasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi itakayo wawezesha kuepukana na mikopo umiza pamoja na kujifunza kuhusu, usimamizi wa fedha binafsi, bima, mikopo, dhamana na uwekezaji.
Hiyo itakuwa awamu ya mwisho ya mfululizo wa programu ya elimu ya fedha kwa umma inayotekelezwa na Wizara ya Fedha ambapo mikoa 13 imefikiwa na kupatiwa elimu hiyo hadi sasa huku Mikoa mingine ikitarajiwa kufikiwa hapo baadae.
Timu hiyo imekutana na wananchi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga na kuwapatia elimu ya fedha ambapo walitoa rai kwa Wizara kuona namna ya kutoa elimu hiyo kwa viongozi ili wawe na uelewa wa pamoja katika kuhudumia wananchi.
Aidha, Timu imetoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mlamleni Kata ya Tambani, Mkuranga na Vikindu ambapo wananchi hao kwa pamoja waliipongeza Wizara kwa jitihada ya kuwafikishia elimu ya fedha na kuomba elimu hiyo itolewe mara kwa mara ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuwa na uchumi jumuishi.