Home KITAIFA MGANGA WA JADI NYASA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI 12 JELA.

MGANGA WA JADI NYASA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI 12 JELA.

Ruvuma

MAHAKAMA ya Wilaya ya Nyasa Septemba, 6 2024 imemtia hatiani Mganga wa Kienyeji Andrea Komba (39) kutumikia kifungo cha miezi 12 au kulipa faini shilingi laki tatu, kwa kosa la kufanya shughuli za uganga bila kibali, kinyume cha sheria namba 45(2)(3) ya sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala 25/2002.

Akisoma hati ya mashtaka D/CPL Anderson mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa, Osmund Ngatunga ameeleza Mshtakiwa ametenda kosa hilo tarehe 03.09.2024 katika eneo ya mchangawedi fukwe za ziwa Nyasa, kijiji cha Mbamba bay Wilayani Nyasa.

Imeelezwa Mahakamani hapo na mwendesha mashtaka kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo maeneo ya Mchangawed mbamba bay wilayani hapa kufanya shughuli za uganga bila kibali na kutosajiliwa na msajili wa Tiba za Asili wala Tiba Mbadala hivyo alimwomba hakimu kutoa adhabu kali kwa kuwa amepotosha jamii.

Alipopewa nafasi ya kujitetea Andrea Komba amekubali kosa na kuomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni mara yake ya kwanza, na anawatoto sita na mke 1 wanaomtegemea.

Akitoa Hukumu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyasa Osmund Ngatunga amesema kwa mujibu wa sheria ya Tiba Asili, Tiba Mbadala Na 25 ya mwaka 2002 imemtia hatiani kutumikia kifungo cha miezi 12 au kulipa faini shilingi laki tatu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here